Aliyekuwa Meneja wa Chama kikuu cha ushirika wa kahawa wilaya ya Mbinga (MBIFACU) Damian Luena akipandishwa kwenye Karandinga la polisi leo katika Mahakama ya Hakimu mkazi wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma kwenda Mahabusu, baada ya kutuhumiwa kukisababishia chama hicho hasara ya shilingi milioni 18.7.
Na Kassian Nyandindi,
|
Mbinga.
HATIMAYE agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa la kutaka kukamatwa na kufikishwa Mahakamani Watuhumiwa wote waliohusika kuhujumu Chama Kikuu cha Ushirika wa Kahawa Mbinga (MBIFACU) Mkoani Ruvuma, limeanza kutekelezwa.
Mpaka sasa Watuhumiwa wawili wamekamatwa na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi Wilaya ya Mbinga Mkoani hapa kwa tuhuma ya wizi wa fedha za chama hicho pamoja na uhujumu uchumi.
Kwa mujibu wa Mwendesha mashtaka wa Polisi, Inspekta Seif Kilugwe alidai mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya hiyo, Magdalena Ntandu kuwa mshtakiwa wa kwanza Frank Ndunguru ambaye ni Mhasibu wa MBIFACU, chini ya kifungu namba 258 na 265 kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 anatuhumiwa kutenda kosa la wizi wa fedha kiasi cha shilingi milioni 6 za chama hicho.
Vilevile katika kosa la pili Mwendesha mashtaka ambaye ni Wakili mwandamizi wa Serikali, Shedrack Kimaro naye alidai mbele ya Hakimu Ntandu kuwa, Damian Luena aliyekuwa Meneja wa Chama hicho cha ushirika anatuhumiwa kwa kosa la kuhujumu uchumi.
Kimaro alidai Mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa Luena baada ya kufanya hivyo alikisababishia chama hicho hasara ya shilingi milioni 18.7 ambapo alitenda kosa hilo mwezi Novemba mwaka 2013 na Juni mwaka 2014, chini ya ibara namba 10 kifungu kidogo cha kwanza jedwali la kwanza na kifungu cha 57 kifungu kidogo cha kwanza namba 60 cha sheria ya uhujumu uchumi sura ya 200.
Baada ya Waendesha mashtaka hao kusoma shtaka hilo katika Mahakama hiyo Hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbinga, Ntandu alisema kuwa Mshtakiwa wa kwanza, Ndunguru dhamana yake ipo wazi lakini hata hivyo alishindwa kukidhi vigezo husika na amepelekwa Mahabusu hadi kesi hiyo itakaposomwa tena Januari 25 mwaka huu.
Hata hivyo kwa upande wa Mshtakiwa wa pili, Luena naye amekosa dhamana kwa kuwa Mahakama hiyo ya Wilaya haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo hadi hapo Mahakama inayoshughulikia ufisadi itakapoketi Januari 25 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment