Na Muhidin Amri,
Tunduru.
MKUU wa Wilaya ya Tunduru Mkoani
Ruvuma, Juma Homera amepiga marufuku Walimu wa shule za Msingi na Sekondari
Wilayani humo kuendelea kuwachangisha Wazazi michango mbalimbali kupitia
wanafunzi wanaosoma katika shule za Serikali.
Aidha Homera amewaonya Walimu hao
kwamba watakaobainika kuendelea na utaratibu wa michango hiyo, watachukuliwa
hatua kali ikiwemo muhusika kufukuzwa kazi kuanzia Mkuu wa shule na Mkurugenzi Mtendaji
wa Halmashauri husika.
Hayo yalisemwa na Mkuu huyo wa Wilaya
wakati alipokuwa akizungumza na Maafisa tarafa, Wakuu wa shule za Sekondari,
Waratibu elimu kata, Watendaji kata na Watendaji wa vijiji katika ukumbi wa
Klasta ya Walimu tarafa ya Mlingoti mjini hapa.
Alisema kuwa hapo awali kulikuwa na michango
ya Madawati, chakula, michango ya Walinzi na mingine mingi ambayo ilionekana
kuwa kero kwa wananchi.
Alieleza kuwa endapo Wazazi au walezi
wa wanafunzi hao watakubaliana wenyewe kuchangisha baadhi ya mchango katika
shule zao, Walimu wasijihusishe na chochote katika upatikanaji wa michango hiyo
ili kuepuka kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti
baadhi ya Wakuu wa shule za Sekondari za kata walisema kuwa michango ya chakula
iliyokuwa ikitozwa ilitokana na makubaliano ya Wazazi wenyewe wenye watoto wao
wanaosoma shuleni ambao wanaishi mbali na makazi yao.
Walimu hao walionesha mashaka kuwa
utaratibu huo huenda ukasababisha utoro wa rejareja kwa wanafunzi na hivyo
kushusha kiwango cha ufaulu katika vipindi vya masomo kwa watoto darasani kwa
sababu hawatakuwa tayari kusoma na njaa.
No comments:
Post a Comment