Saturday, January 27, 2018

SONGEA WANAFUNZI WASIORIPOTI SHULENI KUSAKWA NYUMBA HADI NYUMBA


Na Albano Midelo,       
Songea.

MKUU wa Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma, Palolet Mgema amesema kwamba Oparesheni ya kuwasaka wanafunzi wa madarasa ya awali, msingi na sekondari ambao hawajaripoti shule Wilayani humo itafanyika nyumba hadi nyumba kuanzia sasa ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanaripoti shuleni.
Palolet Mgema.

Alisema uchunguzi umebaini kuwa bado kuna idadi kubwa ya wanafunzi waliotakiwa kwenda shuleni, lakini bado wapo mitaani wakati Serikali inatoa elimu bure kuanzia msingi na sekondari kuhakikisha watoto wote wanapata elimu.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya alieleza kuwa takwimu zinaonesha kuwa wanafunzi wa madarasa ya awali waliopo shuleni hivi sasa ni asilimia 68 tu ya walioandikishwa ambao ni 4,395 kati ya wanafunzi 9,485 waliotarajiwa kuanza elimu ya awali mwaka huu.


Afafanua kuwa katika elimu ya msingi wanafunzi walioripoti darasa la kwanza ni asilimia 81 ambayo ni jumla ya wanafunzi 5,425 ambapo wanafunzi waliotarajiwa kuanza shule ya msingi ni 6,313.

“Hali bado ni mbaya pia hata katika elimu ya sekondari, kwa sababu wanafunzi waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza mwaka huu ni 3,923 hata hivyo walioripoti ni wanafunzi 2,726 hadi sasa sawa na asilimia 69 ni lazima tufanya msako mkali wa kuwatafuta nyumba hadi nyumba ili kujua hawa watoto wapo wapi ili waweze kwenda shule”, alisisitiza.

No comments: