Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WANANCHI wanaoishi katika Halmashauri
ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma, wametakiwa kuendelea kupanda miti rafiki ya
maji kwa wingi hasa kipindi hiki ambacho ni cha mvua za masika katika maeneo
yenye vyanzo vya maji, ili kuweza kuondokana na tatizo la upungufu wa maji
katika kipindi cha kiangazi.
Mwito huo umetolewa jana na Meneja wa
Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (MBIUWASA) katika Mji huo, Patrick
Ndunguru wakati wa zoezi ambalo mamlaka hiyo inaendelea nalo la upandaji miti
kuzunguka vyanzo mbalimbali vya maji ndani ya mji huo.
“Mkakati tulionao wa mamlaka hii ni
kurudisha uoto wa asili katika vyanzo vya maji ambavyo vimeanza kupotea
kutokana na baadhi ya wananchi kuendesha shughuli zao ikiwemo kilimo”, alisema.
Ndunguru alisema kuwa sababu kubwa ya
uharibifu wa mazingira hayo imejitokeza hasa kutokana na wananchi hao
kupendelea kulima kilimo cha bustani kando kando ya mito na kwenye vyanzo vingine
vya maji.
Kadhalika Meneja huyo wa MBIUWASA
amewataka viongozi wa vijiji na mitaa washirikiane na mamlaka hiyo kuhakikisha kwamba
wanakemea hali hiyo na kuwachukulia hatua watu wanaokiuka suala la utunzaji wa
mazingira hasa kwa wale wanaoendesha shughuli za kilimo kwenye vyanzo hivyo ili
kuweza kudhibiti uwezekano wa kupungua kwa maji katika Mji wa Mbinga.
Vilevile ameishukuru Serikali kwa
uamuzi wake uliotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa juu ya kuzuia ujenzi wa
Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga katika eneo la chanzo cha maji Ndengu
ambalo ndiyo tegemeo kwa kuzalisha na kulisha maji wakazi wa Mji huo.
“Kwa kweli Serikali imefanya jambo la
maana sana, kwetu sisi kama mamlaka kuzuia ujenzi wa Ofisi pale katika eneo la
Ndengu endapo ingeruhusu basi kungetokea madhara makubwa ambayo hapo baadaye wananchi
wangetumia maji ambayo sio salama kwa maisha yao”, alisema Ndunguru.
Awali katika kipindi cha mwaka jana,
kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kilipitisha
uamuzi wake wa kujenga Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo katika
kijiji cha Ndengu kata ya Nyoni baada ya kugawanywa na kuanzishwa Halmashauri
ya Mji wa Mbinga.
Hata hivyo imeelezwa kuwa Wajumbe wa kikao hicho
licha ya kupitisha maamuzi hayo hawakutambua umuhimu wa eneo hilo na athari
zinazoweza kujitokeza hapo baadaye kwa kujenga Ofisi na makazi ya watumishi
katika eneo hilo ambalo limehifadhiwa kwa ajili ya vyanzo vya maji.
No comments:
Post a Comment