Na Muhidin Amri,
Madaba.
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma, Shafi Mpenda amepiga marufuku tabia ambayo inafanywa na baadhi ya wakulima wa Wilaya hiyo, wakati wa kuandaa mashamba yao kwa kuchoma moto kwani husababisha misitu mingi ya asili huteketea kwa moto.
Aliwataka wakulima katika jimbo la Madaba kuandaa mashamba kwa njia ya kisasa bila kuathiri mazingira pamoja na viumbe hai wengine hatua ambayo itawezesha kutunza na kuhifadhi mazingira kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo.
Mpenda alisema hayo juzi wakati akiongoza operesheni ya kuwasaka watu wanaojihusisha na ukataji miti ovyo kwa ajili ya shughuli za mkaa, katika kijiji cha Mbangamawe ambacho kimeathirika kutokana na shughuli za uchomaji wa mkaa.
Kwa mujibu wa Mpenda alieleza kuwa misitu mingi ya asili katika jimbo la Madaba imeanza kupotea kutokana na tabia ya uchomaji misitu usiozingatia sheria kwa ajili ya biashara ya mkaa na wengine kwa madhumuni ya kupasua mbao.
Alitaja sababu kubwa ya kupotea kwa misitu ya asili ni uandaaji mashamba kwa njia ya zamani ya kuchoma moto mashamba na imebainika kuwa wapo baadhi ya wakulima pindi wanapoandaa mashamba yao kwa kuchoma moto huo huwashinda na baadaye husambaa hadi msituni na hatimaye kuteketeza misitu iliyohifadhiwa kwa muda mrefu.
Katika kukabiliana na tabia hiyo, Mpenda amewaagiza watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha kwamba wanawachukulia hatua kali za kisheria watu watakaobainika kufanya uharibifu huo.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo wa Madaba ameagiza kila kaya kupanda miti mitano ya matunda na mitano mingine ya kivuli pamoja na mbao kwenye kaya zao ili kuweza kukabiliana na tatizo sugu la ukataji na uchomaji miti ovyo.
No comments:
Post a Comment