Friday, January 12, 2018

UKOSEFU WA FEDHA UNAKWAMISHA UTEKELEZAJI MIRADI YA MAJI MADABA

Na Muhidin Amri,       
Madaba.

MBUNGE wa jimbo la Madaba Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma, Joseph Mhagama amesema kwamba ukosefu wa fedha za kutosha na  baadhi ya wananchi kutopenda kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa miradi ya maendeleo, ndiyo kikwazo kikubwa katika utekelezaji wa miradi ya maji katika baadhi ya vijiji ndani ya jimbo hilo.

Aidha alisema kuwa yeye akiwa ndiye Mbunge wa kwanza wa jimbo hilo kipaumbele chake cha kwanza tangu alipoingia madarakani miaka miwili iliyopita ni suala la upatikanji wa maji safi na salama ambapo alisema atahakikisha kwamba anatafuta fedha kwa ajili ya kumaliza kero hiyo ya maji.

Hayo yalisemwa juzi na Mbunge Mhagama wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu Ofisini kwake huku akisisitiza kuwa bila ushiriki wa wananchi ipasavyo katika ujenzi wa miradi hiyo itakuwa ni ndoto kwa Serikali kuweza kufikia malengo yake.


Alisema kuwa katika jimbo hilo kuna vikundi mbalimbali vilivyoanzishwa na wananchi wenyewe ambao hivi sasa kwa kiasi kikubwa wamefanikisha kuleta huduma ya maji kutoka kwenye vyanzo hadi katika makazi yao hivyo jitihada hizo wanapaswa kuzionesha hata katika miradi ambayo Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi pale inapojengwa.

Amevitaja vijiji vilivyofanya vizuri kupitia vikundi vya watumiaji maji ni Maweso na Lilondo ambako kuna miradi ya maji inayoendelea vizuri na wananchi wa maeneo hayo wameshiriki  kikamilifu wakitambua kuwa ni jukumu muhimu linalopaswa kutekelezwa kwa haraka.

Mbunge huyo aliongeza kuwa kata ya Gumbiro na Mtyangimbole Serikali imekwisha toa fedha kwa ajili ya kazi ya utafiti wa maji na kuwataka wananchi  wa jimbo hilo kushiriki katika shughuli za ujenzi wa miradi ya maji  ili iweze kuwaondolea kero.

Sambamba na hilo Mhagama kwa upande wa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, amewataka wajitume katika kutekeleza majukumu yao ya kazi kwa kushirikiana na wananchi wa jimbo hilo ili Serikali iweze kufanikisha malengo yake.

No comments: