Na Muhidin Amri,
Madaba.
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya
Wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma, Shafi Mpenda amewataka wawekezaji wa ndani na
nje ya nchi kwenda kuwekeza katika maeneo mbalimbali Wilayani humo, kufuatia Halmashauri
hiyo kutajwa kuwa miongoni mwa maeneo yenye fursa nyingi zinazofaa kwa shughuli
za uwekezaji hapa nchini.
Mpenda alitoa wito huo juzi alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na fursa rafiki zilizopo
huko ambazo bado hazijafanyiwa kazi licha ya Wilaya ya Madaba kutajwa kuwa ni
sehemu nzuri kwa shughuli za uwekezaji.
Alisema kuwa Halmashauri hiyo bado kuna
rasilimali nyingi ikiwemo ardhi nzuri yenye rutuba inayofaa kwa kilimo cha
mazao mbalimbali kama vile kahawa, chai, korosho, mahindi tangawizi pamoja na uwepo
wa mto Ruhuji wenye samaki wengi wazuri ambao hawapatikani sehemu yoyote hapa
nchini na misitu mikubwa yenye wanyama kwa ajili ya shughuli za utalii na
uwindaji.
“Madaba inaendelea kukua siku hadi
siku, hata hivyo bado tunakabiliwa na changamoto ya nyumba za kulala wageni,
viwanda nawaomba watu waje kuwekeza katika halmashauri hii”, alisema.
Mkurugenzi huyo aliahidi Serikali
kupitia Halmashauri hiyo itaendelea kuweka mazingira bora na rafiki ya uwekezaji
na wawekezaji na sasa inaendelea kuboresha huduma zote muhimu kama vile huduma
ya maji safi na salama, afya, barabara na huduma za mawasiliano.
Mpenda amewatoa hofu watu wanaohitaji
kuwekeza na kuwaeleza kwamba Madaba ni mahali safi na salama kwa ajili ya
kuwekeza katika miradi ya kiuchumi kama inavyosisitizwa na Serikali ya awamu ya
tano chini ya Rais Dokta John Magufuli.
Katika hatua nyingine Mpenda, amewataka
watumishi wa umma kuongeza juhudi ya kazi pamoja na kutoa ushirikiano kwa watu
wanaokwenda kuwekeza miradi ya kiuchumi huku akisisitiza umuhimu wa wananchi
nao kutumia muda wao kwa ajili ya kufanya kazi za kujiletea maendeleo.
No comments:
Post a Comment