Friday, January 12, 2018

HALMASHAURI WILAYA YA MBINGA KUENDELEA KUBORESHA SEKTA YA ELIMU AFYA

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri Wilaya ya Mbinga, Gombo Samandito akiwa hivi karibuni katika mkutano na baadhi ya wananchi wa kata ya Litembo kuhamasisha shughuli mbalimbali za kimaendeleo.


Na Muhidin Amri,      
Mbinga.

HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma, imepanga kukamilisha kazi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa  116 katika shule za msingi na vyumba 19 kwa upande wa sekondari, katika kipindi cha mwaka 2017/2018.

Aidha halmashauri hiyo  imejenga nyumba 29 za walimu wa shule za msingi na nyumba 12 kwa upande wa sekondari hatua inayotajwa kuwa itaweza kumaliza tatizo la upungufu wa nyumba za kuishi walimu katika halmashauri hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya hiyo, Gombo Samandito alisema pia halmashauri hiyo imekamilisha ujenzi wa matundu ya vyoo 58 katika shule za msingi na matundu manne kwa shule za sekondari.


Alisema kuwa mbali na sekta ya elimu hata kwa upande wa afya wamekarabati zahanati, nyumba za waganga kwenye zahanati tisa, majengo ya utawala matatu katika shule za sekondari, ofisi za walimu msingi 51 na sekondari nane.

Halmashauri ya wilaya ya Mbinga kwa kuzingatia kuwa  umuhimu wa utawala bora kwa kila mtendaji wa Serikali bila kujali wadhifa wake imekarabati ofisi za kata sita na vijiji nne, ili watumishi wake waweze kufanya kazi na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kadhalika hadi sasa alisema kuwa halmashauri hiyo imetumia jumla ya shilingi milioni 460 kati ya shilingi bilioni 1.2 zilizopo kwenye mpango wa kuboresha na kuimarisha majengo ya sekta ya afya na elimu katika vijiji  mbalimbali.

No comments: