Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WADUDU aina ya viwavi jeshi (Fally
arm worms) ambao wameingia katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma, tangu mwezi
Mei mwaka jana mpaka sasa wamefanya uharibifu mkubwa wa mazao na wataalam
husika wamefanikiwa kuwadhibiti kwa asilimia 95.
Afisa Kilimo wa Halmashauri ya
Manispaa hiyo, Zawadi Nguaro alisema kuwa viwavi hao wana uwezo wa kushambulia
aina 80 ya mazao yakiwemo mahindi, miwa na mtama na kwamba tangu walipoingia
katika Manispaa hiyo walianza kwa kushambulia nyasi.
Alisema kuwa wadudu hao waligundulika
mwishoni mwa mwezi Desemba 2017 wakiwa wameshambulia Hekta zaidi ya 1,000 za
mahindi, ambapo wadudu hao hutoboa majani ya mahindi na kuchana kama kamba na
kwamba wana uwezo wa kushambulia kwa kasi kubwa iwapo hawadhibitiwi haraka.
Anayataja maeneo ambayo yaliathirika
zaidi na wadudu hao kuwa ni kata ya Lilambo ambayo Hekta 299 ziliharibiwa, Subira
(250), Tanga (180), Mletele (100), Ruhuwiko (120) Mshangano (50), Matogoro (10),
Ruvuma (26), Seedfarm (20) na Mateka Hekta tano.
Nguaro aliongeza kuwa tangu
walipogundulika wadudu hao idara ya kilimo imekuwa ikitoa elimu na ushauri juu
ya namna ya kupambana nao, ikiwemo matumizi ya viuatilifu vya kukabiliana na
ugonjwa huo ambapo wakulima wamekubali ushauri na kununua viuatilifu hivyo hatimaye
kufanikiwa kupunguza tatizo hilo kwa kiwango kikubwa.
Anavitaja viuatilifu ambavyo vilikuwa
vikitumika katika kukabiliana na wadudu hao kuwa ni MUPA FORCE 720 EC, AGROCRON
720EC, PROTRIN 600 EC, PROSPER 720 EC na DUDUBA 720 EC.
No comments:
Post a Comment