Seleman Jafo. |
Na Lilian Lundo,
Maelezo Dodoma.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Seleman Jafo amewaagiza Wakuu wa
Wilaya na Wakurugenzi wa Halamshauri zote nchini, kuhakikisha kwamba wanajenga
madarasa yenye ubora na viwango vinavyokubalika ili kuondokana na tatizo la
baadhi ya Wilaya kuwa na majengo ya udongo au tembe.
Jafo alitoa agizo hilo leo mjini
Dodoma alipokuwa akifungua mafunzo ya uongozi ya siku tano kwa Wakuu wa Wilaya
na Wakurugenzi toka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara
yanayoendelea kufanyika katika ukumbi wa Hazina Mkoani humo.
“Sitaki kuona madarasa ya udongo,
tembe na watoto kusomea nje hakikisheni matumizi ya mapato ya ndani yanagusa na
kujibu matatizo ya wananchi”, alisisitiza Jafo.
Waziri Jafo aliwataka Wakuu wa Wilaya
kuhakikisha kwamba matumizi ya mapato ya ndani katika Halmashauri zao,
yanatumika katika miradi mbalimbali ya wananchi ikiwemo ujenzi wa madarasa ili
kuondokana na uwepo wa madarasa ya udongo na tembe katika Halmashauri zote hapa
nchini.
Aidha aliwataka Wakurugenzi wa
Halmashauri kufanya maamuzi ya haraka mara wanapopokea fedha za miradi ya
maendeleo, kauli hii imetokana na baadhi ya Wakurugenzi kuwa wazembe katika
kufanya maamuzi hivyo kuchelewesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya
maendeleo katika Wilaya zao na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Naibu Waziri
TAMISEMI Josephat Kandege naye alisema anaamini Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi
hao wataenda kutekeleza yale ambayo watajifunza katika mafunzo hayo.
“Naamini kwa fursa hii ya mafunzo haya
mtakuwa vinara mara mbili au tatu ya mlivyokuwa katika kutekeleza ilani ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM)”, alisema Kandege.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa taasisi
ya uongozi Profesa Joseph Semboja alifafanua kuwa lengo la mafunzo hayo ni
kuimarisha uwezo wa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri katika
kufanya maamuzi ya kimkakati, kuwapa uwezo wa kuongoza watu na rasilimali
nyingine pamoja na kuimarisha uwezo wao katika sifa zao binafsi.
Profesa Semboja alisema awamu hii ya
nne ya mafunzo ya uongozi kwa viongozi hao inakamilisha idadi ya viongozi 324
wa Wilaya na Mamlaka ya Serikali za Mitaa waliotarajiwa kupata mafunzo hayo kwa
nchi nzima.
Mafunzo ya uongozi kwa Wakuu wa
Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri yalizinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa Mei 9 mwaka jana ambapo yameendeshwa kwa awamu tatu tofauti na awamu
hii ya nne ndiyo awamu ya mwisho inayofunga mafunzo hayo kwa viongozi hao wa
Wilaya na Mamlaka ya Serikali za Mitaa.
No comments:
Post a Comment