Na Kassian Nyandindi,
Madaba.
HALMASHAURI ya Wilaya ya Madaba
Mkoani Ruvuma, katika msimu wa mwaka huu inatarajia kupanda miche ya zao la
Korosho 55,020 sawa na ekari 1,965 ya zao hilo ikiwa ni mkakati uliojiwekea
Halmashauri hiyo katika kuongeza vyanzo vyake vya mapato kwa ajili ya maendeleo
ya wananchi.
Shafi Mpenda ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji
wa Halmashauri ya Madaba alisema kuwa pamoja na jitihada hizo Serikali kuu kupitia
Bodi ya korosho Tanzania, imekuwa ikisaidia kuendeleza zao hilo kwa kuleta
mbegu bora, miche iliyobebeshwa, vifaa vya kitalu, viuatilifu na kufanya mafunzo
kwa wakulima wa zao hilo.
Mpenda alieleza kuwa tayari miche
hiyo wamekwisha anza kusambaza kwa wakulima katika vijiji mbalimbali hasa vile
vyenye hali ya hewa inayostawi vizuri korosho ikiwemo kijiji cha Mbangamawe, Ifinga,
Ngadinda, Gumbiro, Lutukila, Mtyangimbole, Magingo, Kipingo na Mahanje.
Alisema kuwa mbali na mikakati waliyonayo
katika kuendeleza kilimo cha zao hilo Halmashauri yake kwa kushirikisha
maafisa ugani waliopo vijijini imejitahidi kusimamia mazao mengine ya biashara
kama vile kahawa na tangawizi huku upande wa mazao ya chakula ikiwemo mahindi, mpunga,
maharage, soya, karanga na mazao ya bustani ambayo hulimwa kwa wingi na kufanya
hali ya chakula kuwa nzuri wilayani humo.
Katika kutekeleza Ilani ya uchaguzi
ya Chama cha Mapinduzi (CCM) alisema kijiji cha Mbangamawe kimefanikisha
kuanzisha Chama cha ushirika cha mazao, ambacho kazi yake kubwa ni
kukusanya mazao toka kwa wakulima na kutafuta masoko, pembejeo za kilimo
na kuziuza kwa wakulima ambo ni wanachama na wale wasiokuwa wanachama.
Mpenda aliongeza kuwa pamoja na
jithada hizo za wakulima na Serikali katika kuendeleza zao la korosho wanakabiliwa
na changamoto ya upungufu wa mbegu za korosho zinazotolewa na Bodi husika
kwani katika msimu wa mwaka huu mahitaji yalikuwa ni miche 130,000 lakini miche
iliyopatikana ni 55,020.
Mbali na mbegu kuwa pungufu pia upatikanaji
wa pembejeo umekuwa ni tatizo kama vile mbolea hazitoshelezi kwani mahitaji ya
wakulima yamekuwa makubwa.
No comments:
Post a Comment