Na Muhidin Amri,
Tunduru.
MKUU wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma,
Juma Homera ametoa agizo kwa shule zote za Msingi na Sekondari Wilayani humo kuhakikisha
wanalima ekari tatu za zao la korosho ikiwa hapo baadaye wakati wa mavuno ndiyo
sehemu ya chanzo kikuu cha mapato.
Aidha alisisitiza kuwa endapo
watazingatia hilo shule hizo zitakuwa na uwezo wa kujipatia fedha na
kujitegemea kutoa hata chakula shuleni kwa wanafunzi wao na kufanya mambo
mengine ya kimaendeleo.
Homera alikemea pia tabia ya baadhi
ya wananchi kwenda kuchukua miche kwenye vitalu ambako imeeoteshwa na kuwauzia
wengine kwa lengo la kujipatia fedha ambapo kwa atakayebainika hatua kali za
kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Agizo hilo lilitolewa juzi wakati
Mkuu huyo wa Wilaya akikagua vitalu vya miche bora ya korosho ambayo
imezalishwa Halmashauri ya Wilaya kupitia vikundi 16 kati ya 18 katika kijiji
cha Nakayaya, Nanyoka na Kangomba ikiwa ndiyo mkakati wa Serikali ya awamu ya
tano katika kuimarisha na kuendeleza zao la korosho hapa nchini.
Wilaya ya Tunduru imezalisha miche ya
korosho 662,163 ambayo wameanza kusambazwa kwa wakulima katika maeneo mbalimbali
hatua ambayo imeelezwa kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ijayo Wilaya
itakuwa na uwezo wa kuzalisha korosho tani 800,000 hadi milioni 1.
Vilevile ameagiza wakulima
kutumia fursa hiyo kuongeza uzalishaji wa zao hilo kwa kuhakikisha miche
wanayopewa wanapeleka katika mashamba yao kwa ajili ya kupanda badala ya
kuingiwa na tama ya kuuza kwa ajili ya kupata fedha.
“Ninaagiza sitaki kusikia miche hii
inauzwa kwa mtu yeyote, Serikali imeanzisha utaratibu huu ili kuweza kuwasaidia
wakulima wetu waweze kujikwamua kiuchumi, kwa hiyo haitakuwa jambo jema kuwakuta
baadhi ya wapuuzi wachache wanatumia nafasi hiyo kukwamisha mpango huu mzuri wa
Serikali ya awamu ya tano”, alisisitiza.
Homera alisema lengo la Serikali Wilayani
Tunduru ni kuona katika kipindi cha miaka mitano ijayo shule zote za msingi na
sekondari Wilayani humo zitoa chakula cha mchana na kuweza kumudu gharama ndogondogo
zenyewe badala ya wakati wote kuitegemea Serikali ambayo ina majukumu mengi kwa
wananchi wake.
Hata hivyo amewataka maafisa kilimo kutokaa
maofisini badala yake wawe wanakwenda mashambani kwa wakulima kutoa elimu na kuwahamasisha
juu ya umuhimu wa kilimo cha korosho ili kuweza kuongeza tija na uzalishaji wa
zao hilo ambalo limeanza kuonekana lina mchango mkubwa kwa kukuza uchumi wa
nchi.
No comments:
Post a Comment