Na Muhidin Amri,
Tunduru.
WAKULIMA wanaozalisha zao la korosho
Wilayani Tunduru Mkoa wa Ruvuma wameipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali
ya Rais Dokta John Pombe Magufuli, kwa uamuzi wake wa kutenga fedha kwa ajili
ya kuboresha na kuimarisha zao hilo kwa kuzalisha miche ambayo
inatolewa bure kwa wananchi.
Walisema kuwa hatua hiyo itahamasisha
wananachi wengi kuanza kulima zao hilo na kuweza kujikwamua na umaskini kwa
kuwa Serikali imeonesha dhamira ya dhati katika kuwasaidia wakulima.
Kwa nyakati tofauti wakizungumza na
mwandishi wetu walisema kuwa hiyo ni hatua nzuri kwa Serikali ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kwani imeonesha ni jinsi gani inavyowajali wananchi wake hasa
kwa kuondoa baadhi ya kero za muda mrefu ambazo zilikuwa zikiwakatisha tama wakulima
na kurahisisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo.
Lwiza Mkuha na Ali Said mbali na
pongezi hizo waliiomba Serikali kuangalia na mazao mengine ikiwemo karanga na
mpunga ambayo yanalimwa na kustawi vizuri katika Wilaya hiyo kwa kutoa mbegu bora
ili kuongeza uzalishaji wake.
Mkuha alisema kuwa walikuwa
hawafahamu kama Halmashauri ya Wilaya imeandaa mpango huo wa kutoa miche bora
ya korosho na kuwataka wakulima wenzake kuchangamkia fursa hiyo ambayo inaonekana
itawaondoa wakulima wa Wilaya ya Tunduru katika umaskini.
Pia amewataka wanawake wengine wa
Wilaya hiyo kuacha kubweteka kwa kuwa tegemezi badala yake waanze sasa kulima
zao la korosho ambalo hapo baadaye litawaondolea aibu na dharau ya wanaume
kwa kuwaita majina mengi ya ajabu ambayo yanawavunjia utu wao.
No comments:
Post a Comment