Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza. |
Na Mwandishi wetu,
Iringa.
SIKU moja baada ya Rais Dokta John Pombe
Magufuli, kupigilia msumari wa mwisho juu ya suala la michango kwa wanafunzi
mashuleni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza amewataka walimu wakuu wa shule
zote Mkoani humo kuandika barua kueleza aina ya michango iliyopo shuleni kwao na
sababu za uwepo wake.
Masenza ameonya mwalimu ambaye atatoa
taarifa za uongo katika barua yake hatua kali zitachukuliwa dhidi yake ikiwemo
ya kuondolewa katika nafasi yake ya kazi.
“Kwenye waraka ambao kila mtu anao
unazungumzia elimu bila malipo, tayari Serikali ilishaelekeza namna ya
kuendesha elimu bila malipo, waraka namba 3 wa mwaka 2016 ambao unazungumzia
elimu bila malipo na waraka wa elimu namba 8 wa mwaka 2011 kuhusu michango
mbalimbali wanayopaswa kutoa wazazi kupitia kamati na bodi za shule,
“Mimi ninajua katika kamati na bodi
za shule ninyi ni makatibu, ikifika katika jambo hili tafadhali kila mwalimu
aone hahusiki na jambo lolote linalozungumzia michango katika shule za msingi
na sekondari na kama kuna hitaji lolote libainishwe na jamii”, alisema Masenza.
Alifafanua kuwa shule ni za jamii na
jamii ikibainisha yenyewe nje ya utaratibu wa mwalimu mkuu juu ya nini wanataka
kufanya na kusimamia wao wenyewe hilo linaruhusiwa.
“Sasa nimewaita ili nijiridhishe,
nitamtaka kila mwalimu mkuu wa shule kwa mkono wake mwenyewe aandike barua ya
kueleza kama shule yake ina mchango ama la na barua zote ziandikwe kwa mkuu wa
mkoa”, alisema.
Masenza alieleza kuwa barua hizo zitapitiwa
na Ofisi yake na kisha ukaguzi utafanyika katika kila shule zikihojiwa kamati
na bodi za shule kubaini michango kama ipo sababu za uwepo na namna amehusika
kuwepo kwa michango hiyo.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa
Mkoa wa Iringa amewaagiza wakuu wa shule kuwapokea wanafunzi wote wanaotarajia
kujiunga na kidato cha kwanza bila kujali wana sare za shule au la.
Katika hatua nyingine amewataka wakuu
wa shule zote za binafsi mkoani humo kuwarejesha wanafunzi waliowaondoa shuleni
mwao kutokana na kutofikia wastani wa ufaulu wanaoutaka la sivyo shule zao
zitafungwa.
No comments:
Post a Comment