Na Mwandishi wetu,
Madaba.
HALMASHAURI ya Wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma, imetoa shilingi milioni 6.2 kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule ya Sekondari Madaba iliyopo wilayani humo, ili kuweza kuwanusuru wanafunzi wanaosoma kwenye shule hiyo waweze kuwa katika mazingira salama.
Aidha imeelezwa kuwa hatua hiyo inafuatia baada ya vyoo wanavyotumia hivi sasa kuwa chakavu na vile vinavyohatarisha maisha ya watoto hao.
Mkuu wa shule hiyo, Humari Mapunda alisema kuwa anaishukuru Serikali kwa uamuzi huo uliochukuliwa na kwamba kwa upande wa ujenzi wa vyoo kwa ajili ya wanafunzi wa kike umekwisha kamilika na mavundi wanaendelea kukamilisha kwa ajili ya wavulana.
Alisema kuwa kazi hiyo wanatarajia kukamilisha haraka iwezekanavyo, ili shule zitakapofunguliwa wanafunzi waweze kutumia vyoo vipya.
Ameomba msaada kutoka kwa wadau mbalimbali wa ndani na nje ya wilaya hiyo, kusaidia fedha na vifaa vya kiwandani kwa kuwa bado wana mahitaji makubwa ya fedha kwa ajili ya kuboresha baadhi ya miundombinu ya shule hiyo kama vile ujenzi wa nyumba za walimu.
Kwa upande wake Kaimu afisa mipango wa halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Mwandishi Nchimbi alisema kuwa malengo yao ni kuhakikisha kwamba katika mwaka wa fedha 2018/2019 wanamaliza changamoto zote zilizopo katika sekta ya elimu, maji, afya na maeneo mengine ili waweze kuboresha huduma.
Alisema kuwa halmashauri kwa kutumia fedha za ndani na zile kutoka Serikali kuu itahakikisha zinatumika vyema kama ilivyokusudiwa ili wananchi waweze kupata huduma bora.
No comments:
Post a Comment