Na Kassian Nyandindi,
Madaba.
MKUU wa Wilaya ya Songea Mkoani
Ruvuma, Palolet Mgema ameongoza Wakulima wa kijiji cha Mbangamawe kata ya
Gumbiro katika Halmashauri ya Wilaya Madaba Mkoani humo, kuzindua mpango maalum
wa kilimo cha zao la korosho kwa kugawa na kupanda miche zaidi ya 55,020 ya zao
hilo.
Akizindua mpango huo Mgema aliwataka Wakulima
wa Madaba kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika mkakati
wa kufufua zao la korosho na mazao mengine makuu ya biashara kama vile pamba, chai,
tumbaku na kahawa.
Alifafanua kuwa Serikali imeamua
kuimarisha zao la korosho hapa nchini baada ya kuonekana limekuwa ni zao ambalo
lina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa na kuharakisha maendeleo ya
mtu mmoja mmoja.
Mgema amewaagiza maafisa kilimo
wahakikishe kwamba wanatumia muda mwingi kuwasaidia wakulima mashambani na sio
kukaa Ofisini kwani wakifanya hivyo itakuwa ni chanzo cha kukwamisha malengo ya
Serikali katika kuinua na kuendelea kuboresha hali ya uzalishaji wa zao hilo.
“Tunampongeza Rais Dokta John Pombe
Magufuli kwa uamuzi wake wa kutoa mbegu za korosho bila malipo kwa wakulima na
sasa tunapaswa kutumia fursa hii kupanda miche kwa wingi ili baadaye tuweze
kuzalisha korosho kwa wingi”, alisema.
Vilevile aliongeza kuwa awali zao la
korosho lilikosa hamasa ya kuendelea kuzalisha kutokana na wananchi wengi
kushindwa kumudu gharama ya pembejeo.
Ameagiza pia maafisa kilimo
wahakikishe kwamba katika msimu huu wa kilimo kila kaya ni lazima wanakuwa na
ekari mbili za shamba la korosho na kwamba aliongeza kuwa kuanzia msimu wa mwaka
huu Serikali inataka kuona mazao yote ya wakulima yanauzwa kwa mfumo wa
stakabadhi ghalani ili wakulima waweze kunufaika kwa kupata soko na bei nzuri ya
uhakika.
Mratibu wa zao la korosho Halmashauri
ya Wilaya ya Madaba, Paschal Umbu naye alieleza kuwa katika msimu wa mwaka huu
wa 2018/2019 wanatarajia kuzalisha tani elfu 57 za korosho kutoka tani 7.441 kwa
msimu uliopita kufuatia mwamko mkubwa wa wananchi kujitokeza katika kulima zao
hilo.
No comments:
Post a Comment