Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida baadhi ya Wakazi wa Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma wamemchongea kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya mji huo, Robert Kadaso Mageni na Watendaji wake ambao wamepewa dhamana ya kusimamia masuala ya usafi ndani ya mji huo kwamba hawawajibiki ipasavyo katika sekta ya usafi.
Tukio hilo la aina yake lilitokea juzi katika uwanja wa michezo uliopo Mbinga mjini, wakati Waziri huyo alipokuwa akisikiliza kero mbalimbali za wananchi.
Wakazi hao kwa nyakati tofauti walieleza kuwa kumekuwa na uzembe mkubwa wa kutosimamia masuala ya usafi kikamilifu katika mji huo, ikiwemo uzoaji taka kwenye maghuba yaliyopo mjini hapa ambapo wakati mwingine taka zimekuwa zikikaa kwa siku nyingi bila kuzolewa jambo ambalo ni hatari kwa afya zao.
Maghuba hayo ambayo yamejengwa katika makazi ya watu, walifafanua kuwa hasa kipindi hiki cha masika endapo hazizolewi kwa wakati, zimekuwa zikitoa harufu kali na kuwa kero katika jamii.
Baada ya Waziri Mkuu Majaliwa kusikiliza kero hizo alimtaka Mkurugenzi mtendaji wa mji huo, Mageni kujibia jambo hilo ambapo hakujitokeza na badala yake alipojitokeza Afisa afya wa mji huo, Felix Matembo alisema kuwa tatizo kubwa linalowafanya washindwe kukusanya taka hizo kwa wakati ni kutokana na kukosa vifaa vya kutosha vya kuzolea taka kama vile magari (Lori).
"Mheshimiwa Waziri katika mji huu uzalishaji wa taka umekuwa mkubwa kwa siku taka zinazozalishwa hapa ni tani 18 mpaka 21 na sisi tuna Lori moja tu la kuzolea taka ambalo halikidhi mahitaji", alisema Matembo.
Kwa upande wake Waziri Mkuu, Majaliwa alisema kuwa kutokana na hali hiyo kuna kila sababu kwa Watendaji wa mji huo ambao wamepewa dhamana ya kusimamia masuala ya usafi kukaa pamoja na viongozi wa Serikali za mitaa waratibu vizuri jambo hilo ili kuweza kumaliza kero hiyo.
"Wewe unajua una lori moja tu la kuzolea taka halafu unawaambia watu bado waendelee kurundika taka, sasa nataka nisikie baraza lenu la Madiwani linaweka utaratibu mzuri wa kuuweka mji katika hali iliyokuwa safi, watumieni kwa kuwaajiri watu watakaoweza kufanya kazi hii kwa ufanisi", alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
No comments:
Post a Comment