Na Kassian Nyandindi,
Songea.
ANDREW Kuchonjoma ambaye ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi
wa Habari mkoani Ruvuma (RPC) amewataka wanachama wake ndani ya klabu hiyo,
kujiendeleza kielimu katika tasnia ya habari ili waweze kufanya kazi zao kwa
urahisi, katika ulimwengu huu wa sayansi na tekinolojia.
Sambamba na hilo alieleza kuwa kuna kila sababu kwa mwandishi
wa habari kuzingatia maadili ya taaluma hiyo, wakati wa kutekeleza majukumu ya
kazi zake ya kila siku hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, ili kuweza
kuepukana na matatizo au migogoro inayoweza kujitokeza baadaye.
“Ndugu zangu kusoma ni jambo muhimu sana ambalo tunapaswa
kulipatia kipaumbele, hapa Ruvuma kuna chuo cha habari ambacho nawashauri
wenzangu tujiunge na tuweze kupata fursa ya kujiendeleza kielimu tusiishie
kukaa tu bila kuwa na mawazo mapya ya kujiendeleza kielimu, katika taaluma hii
tuliyonayo”, alisema Kuchonjoma.