Friday, February 9, 2018

ASILIMIA 54 TASAF MANISPAA SONGEA WANALIPWA KWA NJIA YA MTANDAO

Baadhi ya Wanufaika wa TASAF mtaa wa Mtendewawa Manispaa ya Songea wakipokea fedha za Ruzuku zinazotolewa na mfuko huo kwa kaya maskini.


Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma, imeanza kutoa malipo kwa njia ya Mtandao kwa kaya maskini zipatazo 4,880 zilizopo katika mpango wa kunusuru kaya maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Mratibu wa Mfuko huo katika Manispaa hiyo, Christopher Ngonyani alisema kuwa kati ya kaya hizo kaya 2,638 sawa na asilimia 54 zinapokea fedha kwa njia ya mitandao ya simu na kaya 2,242 sawa na asilimia 46 bado zinapokea fedha kwa njia ya fedha taslimu. 

Alisema kuwa katika kipindi cha mwezi Januari hadi Februari mwaka huu kaya 2,242 zimelipwa fedha taslimu zaidi ya shilingi milioni 88 na kaya 2,638 zimelipwa kwa mtandao zaidi ya shilingi milioni 88 na kufanya jumla ya zaidi ya shilingi milioni 176 zimetolewa kwa wanufaika wote katika kipindi hicho.


“Lengo ni kwamba ifikapo mwezi Juni mwaka huu tunatarajia kufikia asilimia 90 ya wanufaika wote wa TASAF kulipwa fedha kwa njia ya mtandao”, alisema Ngonyani.

Vilevile alisema kuwa lengo la Serikali kuanzisha malipo kwa njia ya mtandao ni kuweza kurahisisha usafirishaji wa fedha kwa usalama wa hali ya juu, kufikisha fedha kwa wakati kwa walengwa na kupunguza gharama za uendeshaji wa mradi.

Ngonyani alifafanua kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha wanufaika wote wanajisajili kulipwa kwa njia ya mitandao ili kuepukana na changamoto nyingi ambazo zinaweza kujitokeza katika malipo ya fedha taslimu ikiwemo kutolewa kwa malipo hewa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea, Palolet Mgema akizungumza na wanufaika hao katika mtaa wa Mitendewawa Kata ya Mshangano Manispaa ya Songea Mkoani hapa, alisema Serikali iliamua kuanzisha mfumo huo wa ruzuku kwa kaya maskini ili kuweza kumkomboa mwananchi mwenye maisha duni.

Mgema alisema hivi sasa asilimia kubwa ya wanufaika wameweza kujiingiza katika shughuli za uzalishaji mali ikiwemo ufugaji na biashara ndogo ndogo.

Kadhalika Mkuu huyo wa Wilaya anazitaja changamoto ambazo zimejitokeza kwa baadhi ya wanufaika wachache Wilayani humo, kuwa ni pamoja na kutumia fedha wanazozipata kwa masuala ya mambo ya anasa ikiwemo kunywa pombe, hali ambayo inarudisha nyuma azma ya Serikali ya kuzikomboa kaya hizo.

Utafiti uliofanywa katika mitaa mbalimbali ya Manispaa ya Songea ambayo wanufaika wamelipwa kwa njia ya mtandao, tumebaini kuwa mfumo huo umepata mafanikio makubwa baada ya wanufaika wengi kupata fedha zao mapema na kwa haraka, hali ambayo imesababisha wanufaika ambao bado hawajajisajili kwenye mfumo huo kuhamasika kwenda kujisajili.

Manispaa hiyo ni moja kati ya Halmashauri 16 nchini zilizochaguliwa kufanya majaribio ya malipo kwa njia ya mtandao wa simu, kwa wanufaika wa Mfuko huo wa maendeleo ya jamii ili kuepukana na changamoto zilizokuwa zimejitokeza kwa kutumia mfumo wa kulipwa fedha za taslimu.

Kwa ujumla mpango huu wa kunusuru kaya maskini unaendeshwa katika Halmashauri 163 nchini na kwamba umeweza kunufaisha kaya maskini zikiwemo zile ambazo awali zilikuwa zinapata mlo mmoja kwa siku ambapo hivi sasa zinaweza kupata milo mitatu kwa siku.

No comments: