Wednesday, February 7, 2018

KIPINDUPINDU CHATOKEA MBINGA NA KUATHIRI WATU 28 KIJIJI CHA ULIMA UKATA



Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

MLIPUKO wa Ugonjwa wa Kipindupindu umetokea katika kijiji cha Ulima, kata ya Ukata Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma na kuathiri watu 28 Wakazi wa kijiji hicho, ambao wote wamenusurika kupoteza maisha baada ya timu ya wataalamu kuwahi kutoa tiba katika eneo la tukio.

Taarifa zilizomfikia Mwandishi wetu kutoka kwa Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya hiyo, Hussein Sepoko alisema kuwa tukio la ugonjwa huo liliambatana na watu hao kuugua vimelea vilivyoambatana na dalili za kuhara na kutapika, ambapo kati ya hao wagonjwa 19 walikuwa wanawake na 9 wanaume.

Sepoko alisema kuwa chanzo kikubwa cha ugonjwa huo kilitokana na kuchafuliwa kwa vyanzo vya maji na uhaba wa vyoo katika kijiji hicho, ambapo wananchi wengi wamekuwa wakitumia mto uliopo kijijini humo ambao ndiyo mpaka unaotenganisha Wilaya ya Mbinga na Nyasa.


Alisema kuwa maji ya mto huo wananchi hao wamekuwa wakiyatumia kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kunywa, bila hata kuyachemsha licha ya watu kupewa elimu juu ya umuhimu wa kuzingatia usalama wa afya zao.

Pia alifafanua kuwa kumekuwa na uhaba wa vyoo katika kaya nyingi ambazo wamezitembelea na kujionea hali hiyo, ikiwemo hata shule ya msingi Ulima iliyopo katika kata hiyo imekuwa na uhaba wa matundu ya vyoo hali ambayo inawafanya wanafunzi wengi kujisaidia porini.

Vilevile tatizo la unawaji wa mikono baada ya kujisaidia nalo imekuwa ni changamoto kubwa huku wengi wao walikiri kutonawa wakitoka kujisaidia na wengine hutumia maji, yaliyopo kwenye chanzo cha mto kujisafisha huku maji hayo yakitumika na wengine ndiyo maana imetokea kwa urahisi kusambaa kwa ugonjwa.

Mganga huyo alieleza kuwa uongozi wa Wilaya ya Mbinga ulipopata taarifa juu ya hilo timu ya wataalamu wa afya ipo huko mpaka sasa ikiendelea kuhudumia wananchi kwa kuwapa maelekezo ya aina mbalimbali namna ya kujikinga na kuepukana nao.

Kadhalika wagonjwa hao waliobainika walipelekwa katika zahanati ya misheni Lundomato iliyopo Wilayani humo na kupatiwa matibabu kwa haraka ambapo wataalamu hao wameenda huko na vifaa tiba na kuweza kuendelea kuokoa maisha ya waathirika hao.

Hata hivyo mpaka sasa hakuna vifo vilivyotokea na kwamba sampuli zilizochukuliwa kwa wagonjwa hao kwa njia ya haja kubwa na kupelekwa katika maabara ya Mkoa wa Ruvuma kwa utambuzi zaidi bado zinathibitisha kuwa wagonjwa hao wanaugua Kipindupindu.

No comments: