Sunday, February 18, 2018

DOKTA MAGUFULI ASIKITISHWA KIFO CHA MWANAFUNZI AKWILINA SERIKALI KUGHARIMIA TARATIBU ZA MAZISHI

Dokta John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Na Mwandishi wetu,

DOKTA John Pombe Magufuli, ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa kauli yake akizungumzia juu ya kifo cha mwanafunzi aliyepigwa risasi na Polisi, Februari 16 mwaka huu.

Katika ukurasa wake wa twitter, Rais Magufuli ameandika ujumbe kuhusu kusikitishwa kwake na kifo cha Akwilina Akwiline na kuagiza vyombo vya dola kuwachukulia hatu waliohusika kufanya hivyo.

“Nimesikitishwa sana na kifo cha mwanafunzi Akwilina Akwiline wa Chuo cha Usafirishaji (NIT),


“Natoa pole kwa familia, ndugu, wanafunzi wa NIT na wote walioguswa na msiba huu,

“Nimeviagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua za kisheria waliosababisha tukio hili”, ameandika Rais Magufuli.

Kwa ujumla Akwilina alikuwa mwanafunzi wa Chuo hicho jijini Dar es salaam, ambapo aliuawa kwa kupigwa risasi na Polisi wakati wa vurugu za siasa zilizotokea siku ya Ijumaa, akiwa kwenye daladala.

Kuhusu Mazishi

Serikali imetangaza kugharamia mazishi ya mwanafunzi huyo aliyeuawa kwa kupigwa risasi, wakati wa maandamano ya wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakishinikiza Mkurugenzi wa Uchaguzi Kinondoni kutoa viapo kwa mawakala wa chama hicho.

Juu ya kugharimia mazishi hayo kauli hiyo imesemwa leo Februari 18 mwaka huu na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
salaam.

“Serikali imepata pigo kwani inawekeza fedha nyingi kusomesha wanafunzi na marehemu Akwilina alikuwa ni miongoni mwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu, tutagharamia shughuli zote za mazishi ya marehemu hadi atakapopumzishwa katika makao yake ya milele”, alisema Profesa Ndalichako huku akitoa onyo kwa Watanzania kuhusu kutofanya maandamano.

“Nawasihi Watanzania kujiepusha na maandamano na vitendo vyote ambavyo vinaweza kusababisha uvujifu wa amani”, alisema.

No comments: