Tuesday, February 20, 2018

SERIKALI YATOA SOMO KWA WALIMU SHULE ZA SEKONDARI NCHINI



Na Mwandishi wetu,

SERIKALI imesema kuwa Mwalimu wa shule ya Sekondari kufundisha shule ya Msingi, maana yake sio kwamba kushushwa cheo na kwamba jambo hilo sio la ajabu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa kitengo cha mawasiliano Ofisi ya Rais (Utumishi), Florence Lawrence imesema kuwa Serikali kuwapangia baadhi ya walimu wa Sekondari kufundisha shule za Msingi ni moja ya hatua za kuongeza ufanisi na kuleta mgawanyo sawa wa walimu katika shule hizo.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dokta Laurean Ndumbaro amenukuliwa katika taarifa hiyo ambayo ilitolewa leo Februari 20 mwaka huu.


Alisema hatua hiyo haimaanishi kuwa walimu wanaotoka kwenye shule ya Sekondari kwenda kufundisha Msingi wameshushwa cheo.

Dokta Ndumbaro alitoa ufafanuzi huo katika kikao kazi na Watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Makambako.

Alisema lengo la Serikali ni kuondoa upungufu wa walimu katika shule za Msingi na kuimarisha utoaji wa elimu.

Katibu Mkuu huyo ameainisha kuwa sifa za kufundisha na kiwango cha elimu zinaendana na mabadiliko yanayotokea duniani, hivyo mwalimu mwenye elimu ya kiwango cha Shahada ya kwanza kufundisha shule ya Msingi isionekane ni jambo la ajabu.

Pamoja na mambo mengine, Dokta Ndumbaro amewaambia Watumishi wa umma kuwa, maendeleo katika sekta yoyote, ikiwamo ya elimu yanakuja na mabadiliko hivyo wayapokee na kufanya kazi ili kuweza kufikia lengo.

No comments: