Wednesday, February 21, 2018

MANIAMBA SONGEA KUCHIMBWA MAKAA YA MAWE MIAKA 40 WANANCHI 600 KUPATA AJIRA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira na Walemavu Jenista Mhagama wa pili upande wa kulia akiangalia kipande cha mkaa wa mawe wakati alipotembelea mgodi wa utafiti wa makaa ya mawe wa Kambas Group Of Companies katika kijiji cha Maniamba kata ya Muhukuru Wilaya ya Songea, wa kwanza upande wa kushoto ni Mwenyekiti wa Kambas Group of Companies Yahaya Yusuf na upande wa kulia ni Mhandisi wa madini wa Kampuni hiyo, Timoth Malima.


Na Mwandishi wetu,           
Songea.

WANANCHI zaidi ya 600 wa kutoka katika vijiji mbalimbali Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma, wanatarajia kupata ajira katika mgodi wa makaa ya mawe uliopo kwenye kijiji cha Maniamba kata Muhukuru Wilayani humo, ambao unatarajiwa kuanza shughuli zake za uchimbaji wakati wowote kuanzia sasa.

Kampuni ya Kambas Group of Companies ambayo imeanza shughuli ya utafiti wa madini hayo tokea mwaka 2017 na kubaini uwepo wa makaa kiasi cha takribani tani milioni 20 ambapo baada ya kukamilisha utafiti huo yataweza kuchimbwa kwa muda wa miaka 40 kwa uzalishaji wastani wa tani 500,000 kwa mwaka.

Yahaya Yusufu ambaye ni Mwenyekiti wa Kampuni hiyo alisema hayo juzi kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge Ajira na Walemavu Jenista Mhagama wakati Waziri huyo alipokuwa ametembelea kujionea shughuli zinazoendelea kufanyika katika mgodi huo ambapo Mhagama alikuwa katika ziara yake ya kuhimiza, kuangalia na kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za kimaendeleo katika jimbo lake la Peramiho Wilayani hapa.


Kwa mujibu wa maelezo ya Mwenyekiti huyo alieleza kuwa Kampuni ya Kambas mara baada ya kukamilisha utafiti na kuanza rasmi uchimbaji wa madini hayo, inatarajia kuongeza wigo wa ajira hasa kwa Wakazi wanaozunguka katika eneo ulipokuwa mradi na kwamba shughuli zitakazokuwa zinafanywa hapo zitahusisha makundi ya watu wenye elimu inayohitaji sifa mbalimbali na wale wasiokuwa na elimu.

Alisema kuwa Kampuni wakati wote itajitahidi kufanya kazi kwa kushirikiana karibu na Serikali katika kuboresha maendeleo na kuimarisha mahusiano katika jamii ikiwemo kusaidia kutoa huduma mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Ofisi ya kata, zahanati ya kijiji na baadhi ya madarasa ya shule ya msingi.

Pamoja na mambo mengine alizungumzia pia changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo ubovu wa barabara kutoka Muhukuru barabarani hadi eneo ulipokuwa mradi sawa na urefu wa Kilometa 6 kwani barabara hiyo sio nzuri inahitaji matengenezo ili kuwezesha magari makubwa kupita.

Yusufu ameiomba Serikali isaidie kuimarisha barabara hiyo ili iweze kupitika wakati wote na kuweza kurahisisha katika kusafirisha makaa ya mawe yatakayokuwa yanachimbwa huko.

Mara watakapokuwa wanaanza shughuli za uchimbaji Halmashauri ya Wilaya ya Songea itaweza kupata asilimia 3 ya mapato yatokanayo na shughuli za uchimbaji huo kwa kila mwezi na ukusanyaji wa ushuru shilingi 1,000 kwa kila tani ya makaa yatakayopatikana na kusafirishwa.

No comments: