Sunday, February 18, 2018

KUKAMILIKA UJENZI WA DARAJA MTO NANYUNGU TUNDURU KUMALIZA KERO ZA WANANCHI

Daraja  linalojengwa na Serikali chini ya Wakala wa ujenzi Mjini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Tunduru, kwa gharama ya shilingi bilioni 115.804 lenye urefu wa mita 45 katika mto  Nanyungu kijiji cha Fundimbanga Wilayani humo kama linavyoonekana katika picha ambapo kukamilika kwake kutasaidia kukua kwa maendeleo  ya wananchi wa Wilaya hiyo.


Na Kassian Nyandindi,    
Tunduru.

UJENZI wa daraja kubwa la kisasa katika mto Nanyungu litakalounganisha kijiji cha Fundimbanga na vijiji vingine Wilayani Tunduru Mkoa wa Ruvuma, limeanza kujengwa ili kuweza kuondoa kero mbalimbali zilizodumu kwa muda mrefu ambazo walikuwa wakipata wananchi wa Wilaya hiyo.

Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) Wilayani hapa, ndiye ambaye ameanza kazi ya usimamizi wa ujenzi huo na kwamba kukamilika kwa daraja hilo, imeelezwa kwamba kutarahisisha mawasiliano kati ya pande hizo mbili kwa maeneo ya vijiji hivyo.

Meneja wa TARURA Wilaya ya Tunduru, Mhandisi Cyprian Kimwaga alisema kuwa kujengwa na kukamilika kwa daraja hilo kutamaliza pia kero ya wananchi kuvuka kwa kutumia daraja la miti lililopo katika mto huo.


Kimwaga alifafanua kuwa kuvuka katika daraja hilo la miti kumekuwa kukihatarisha usalama wa maisha ya wananchi hasa kipindi cha masika wakihofia kusombwa na maji au kuliwa na mamba kutokana na mto huo kuwa na mamba wengi.

Alisema kuwa Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 115.804 kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa mita 45 ambapo ni kati ya madaraja makubwa, Wilayani humo na  linatajwa kuwa ndiyo mradi mkubwa kutekelezwa na TARURA katika Mkoa wa Ruvuma tangu Serikali ilipoanzisha Wakala huyo.

Daraja hilo linajengwa na Kampuni ya kitanzania inayofahamika kwa jina la IBIHI chini ya usimamizi wa TARURA ambapo kampuni  hiyo imeonesha uwezo mkubwa ambao daraja hilo linatarajiwa kukamilika ifikapo Mei 28 mwaka huu na sasa ujenzi wa nguzo umekamilika kabla ya kuendelea na kazi nyingine.

Vilevile kukamilika ujenzi wake wananchi wanaozalisha mazao ya biashara na chakula ikiwemo korosho, mahindi na zao la mpunga litawezesha pia waweze kufanya shughuli zao za biashara na kuharakisha kukua kwa uchumi wao na Wilaya kwa ujumla.

Kadhalika kwa upande wao wakizungumzia ujenzi wake baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Tunduru, Vumilia Lipapapa na Bahati Mtweve wameishukuru Serikali kwa uamuzi iliochukua wa kulijenga daraja katika mto Nanyungu wakieleza kuwa litasaidia wafanye shughuli zao za maendeleo kwa ufasaha ikiwemo kati yao na watu wengine wa maeneo mengine.

Vumilia Mtweve alisema kuwa litaweza kumaliza tatizo kwa akina mama wajawazito na wagonjwa wengine hasa pale wanapougua na kubebwa kwa kutumia matenga, pale wanapokwenda hospitali kwa ajili ya kupata matibabu kwani hapana usafiri mwingine unaoweza kupita katika daraja hilo la miti.

“Kwa kweli tunaishukuru Serikali yetu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa uamuzi wake wa kujenga daraja hili, tunaamini litakapokamilika tutaondokana na kero hii ya wagonjwa wetu kubebwa katika matenga kwa kutumia baiskeli hasa kwa akina mama wajawazito wanapofikia hatua ya kujifungua”, walisema.

No comments: