Wednesday, February 28, 2018

NJALAMATATA NAMTUMBO WAKOSA MAHALI PA KUISHI BAADA YA NYUMBA ZAO KUEZULIWA NA UPEPO MKALI

Hii ni moja kati ya nyumba ambayo imeezuliwa na upepo mkali ulioambatana na mvua katika kijiji cha Njalamatata kata ya Mkongo Nakalawe Wilayani Namtumbo Mkoani Ruvuma.


Na Yeremias Ngerangera,    
Namtumbo.

UPEPO mkali uliokuwa umeambatana na mvua katika kijiji cha Njalamatata kata ya Mkongo Nakalawe Wilayani Namtumbo Mkoa wa Ruvuma, umeleta maafa kwa baadhi ya wakazi wa kijiji hicho kuezuliwa nyumba zao na kukosa mahali pa kuishi.

Tukio hilo limetokea juzi majira ya mchana baada ya nyumba tano kuezuliwa kwenye kijiji hicho na kufanya wakazi hao, wakibaki wanahangaika kutafuta mahali pa kujihifadhi kwa majirani zao.

Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya hiyo ikiwa imeongozana na Katibu tawala wa Wilaya ya Namtumbo, Adelin Nchimbi walikwenda katika eneo hilo la tukio na kuzungumza na waathirika ambao nyumba zao zimebomolewa na upepo huo uliokuwa umeambatana na mvua hiyo.


Walipofika katika eneo la tukio Kamati hiyo ilishuhudia nyumba tano zikiwa zimeezuliwa katika kijiji hicho cha Njalamatata, lakini hapa kujitokeza mwananchi yeyote aliyejeruhiwa.

Kamati  hiyo iliweza kubaini kwamba hasara hiyo iliyojitokeza ilitokana na nyumba hizo kujengwa chini ya kiwango.

Akizungumza na waathirika hao katika eneo la tukio Katibu tawala wa Wilaya ya Namtumbo, Nchimbi alitoa msisitizo na kuwaelekeza wakazi hao kuzingatia ubora na taratibu husika wakati wanapojenga nyumba zao ili wasiweze kupata hasara kama hiyo.

Pamoja na mambo mengine, wananchi walioathirika ni Clavery Ponera, Donatus Kapinga, James Mdagi, Sadick Kapinga, Rusti Kimbili na Lotary Hongo ambao wote ni wakazi wa kijiji hicho Wilayani hapa.

No comments: