Wednesday, February 28, 2018

WATUMISHI WAZEMBE HALMASHAURI WILAYA MBINGA KUENDELEA KULA KIBANO

Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma, Gombo Samandito amesema kuwa amesikitishwa na utendaji kazi wa Ofisi ya Msimamizi na mdhibiti ubora wa elimu Wilayani humo kwamba Watendaji wa Ofisi hiyo, wamekuwa hawatekelezi majukumu yao ya kazi ipasavyo.
Gombo Samandito.

Samandito alieleza kuwa kutokana na hali hiyo anajiona kama vile anapwaya katika utendaji wake, hivyo atatoa kibano kwa wale wote ambao ni wazembe katika kazi.

Mkururugenzi huyo alisema hayo juzi baada ya kupokea taarifa ya hali ya ukaguzi wa maendeleo ya elimu ya Msingi na Sekondari katika kikao cha tathimini ya elimu kilichofanyika mjini hapa.

Alisema kuwa kumekuwa na visingizio ambavyo havina msingi wowote kwamba Ofisi hiyo inashindwa kutekeleza kikamilifu majukumu yake ya kazi kutokana na kukosa fedha na gari ili waweze kutimiza ipasavyo uendeshaji wa shughuli zao za kila siku.


“Nimesikitishwa sana na hawa watu wa ubora wa elimu, mimi sihitaji visingizio kama hivi ambavyo havina faida yoyote katika jamii, nimekuwa nikisaidia kutoa magari na mafuta kwa shughuli nyingi tu hapa Wilayani,

“Lakini toka nimeanza kufanya kazi hapa Mbinga sijawahi kuwaona hawa watu Ofisini kwangu na kunieleza au kuniandikia matatizo yao yanayowakabili, kibano ni kitu namba moja kwangu naanzia na maafisa elimu msingi hadi sekondari”, alisisitiza Samandito.

Aliendelea kusisitiza kuwa ufaulu wa masomo umekuwa ukishuka mashuleni kutokana na uzembe unaofanywa na Ofisi hiyo ya msimamizi na mdhibiti wa elimu Wilayani hapa, kutotimiza majukumu yao ya kazi hivyo yeye akiwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo atawachukulia hatua wale wote ambao ni wazembe kabla yeye hajaharibikiwa.

Aliongeza kuwa sababu nyingine inayoleta vikwazo kwa watoto mashuleni kutosoma vizuri na kuzingatia masomo yao, hali hiyo inatokana na zaidi ya asilimia 90 baadhi ya viongozi wenye jinsia ya kiume wakiwemo Waratibu elimu kata, Walimu wakuu na viongozi wengine Wilayani Mbinga wamekuwa wakiwatongoza wanafunzi wao na kufanya nao mapenzi hatimaye huwafanya wanashindwa kuzingatia vizuri masomo yao wanapokuwa darasani. 

Pamoja na mambo mengine, alisisitiza kuwa itakuwa ni aibu endapo vitendo hivyo havitakomeshwa haraka na kuhakikisha ufaulu katika masomo kwa watoto mashuleni, unaendelezwa kikamilifu kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye na kwamba hata wale watumishi wazembe katika sekta nyingine zilizopo ndani ya Halmashauri hiyo watachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kushushwa cheo au kufukuzwa kazi.

No comments: