Friday, February 9, 2018

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA ZA KISHERIA WANAOUZA MBOLEA BEI JUU MBINGA


Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

SERIKALI Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma, imetoa onyo kali kwa Wafanyabiashara wanaojishughulisha na uuzaji wa Mbolea ya kukuzia mazao shambani Wilayani humo, kuzingatia bei elekezi iliyotolewa na Serikali na sio vinginevyo.

Mhandisi Gilbert Simya.
Aidha imeelezwa kuwa msako mkali unaendelea kufanyika ili kuweza kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria, watu wanaodaiwa kuficha mbolea ya ruzuku ambayo ni ya kukuzia mazao aina ya UREA na baadaye huuza bei ya juu kwa wakulima tofauti na maelekezo yaliyotolewa na Serikali.

Katibu tawala wa Wilaya hiyo, Mhandisi Gilbert Simya alisema hayo leo wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari Ofisini kwake juu ya tatizo la uhaba wa mbolea za kukuzia mazao shambani lililopo Wilayani hapa.


Simya alifafanua kuwa mahitaji ya mbolea aina hiyo katika Wilaya ya Mbinga hivi sasa yamekuwa makubwa ambapo maafisa kilimo wanafanya tathimini, ili kujua ni kiasi gani halisi kinatakiwa kutokana na uzalishaji uliopo hivyo kila mfanyabiashara anapaswa kuuza kwa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Serikali.

Alisema kuwa kuanzia Februari Mosi mwaka huu bei mpya ya mbolea aina ya UREA ambayo imetolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ni kwamba mfuko wenye kilo 50 kwa Halmashauri ya Mji wa Mbinga unapaswa kuuzwa kwa shilingi 56,585, kilo 25 unauzwa kwa shilingi 30,293, kilo 10 unauzwa shilingi 12,117 na kilo 5 inabidi uuzwe kwa shilingi 6,459.

Vilevile akifafanua kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mfuko wa kilo 50 nao unauzwa kwa shilingi 57,149, kilo 25 shilingi 30,575, kilo 10 shilingi 12,230 na kwamba kilo 5 unauzwa kwa shilingi 6,515.

“Bei ya jumla ambayo Wakala wa Mkoa mzima kwa mfuko wa UREA wa kilo 50 popote pale anapaswa kuuza kwa shilingi 52,824 na kila mkulima nasisitiza anapouziwa mbolea apewe risiti ya Serikali (EFD)”, alisema Simya.

Hata hivyo kwa upande wao baadhi ya wakulima wa Wilaya hiyo kwa nyakati tofauti wamelalamikia kuuziwa mbolea aina ya UREA kwa bei ya juu na baadhi ya wafanyabiashara Wilayani humo, jambo ambalo Serikali ya Wilaya imethibitisha kupokea malalamiko hayo na kueleza kuwa yanafanyiwa kazi na wahusika watakapobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.

No comments: