Friday, February 23, 2018

PROFESA NDALICHAKO KUMSOMESHA MDOGO WAKE AKWILINA MPAKA CHUO KIKUU



Na Mwandishi wetu,

ULINZI na Usalama umeimarishwa katika eneo alilozikwa mwanafunzi wa chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline katika kijiji cha Olele Wilayani Rombo.

Mwandishi wetu ambaye aliwasili katika eneo la tukio leo Ijumaa wakati mazishi ya mwanafunzi huyo yanafanyika, alibaini uwapo wa askari wengi wakiwamo wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na askari kanzu.

Mbali na askari kanzu, walionekana maofisa usalama wa Taifa na Polisi waliovalia kiraia, wakiwa wameegesha magari kimkakati, mita kati ya 100 hadi 150 kutoka nyumbani kwa wazazi wa marehemu.


Vilevile Ofisa mnadhimu wa Polisi namba moja wa Mkoa Kilimanjaro, Koka Moita, ambaye alizoeleka kuwa katika sare, alionekana akitembea kwa miguu mitaani akiwa amevalia kiraia.

Moita alipoulizwa kuhusu usalama, alikiri kuna ulinzi wa kutosha lakini alisema anayeweza kuzungumzia hilo ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah.

Pia walikuwa mgambo ambao wameshika doria maeneo ya maegesho ya magari ya wageni mbalimbali na eneo la Kanisa ilipofanyika ibada.

Askari wa usalama barabarani nao walionekana barabara kuu ya Olele-Useri, wakisimamia usalama wa watembea kwa miguu na watumiaji wengine wa barabara, jirani na shughuli za mazishi zilipofanyika.

Waziri wa Elimu

Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako aliahidi kumsomesha mdogo wake Akwilina Akwilini, ambaye ni Angela Akwilini na hivi sasa anasoma kidato cha tatu.

Akizungumza baada ya mazishi ya Akwilina aliyeuawa kwa kupigwa risasi Februari 16, mwaka huu eneo la Mkwajuni jijini Dar es Salaam, Profesa Ndalichako alisema atamsomesha Angela hadi Chuo Kikuu.

Pamoja na mambo mengine, Akwilina Akwiline katika safari yake ya mwisho hapa duniani, amezikwa katika makaburi ya kijijini kwao Olele Wilayani Rombo.

No comments: