Tuesday, February 6, 2018

MWENYEKITI WA CCM WILAYA YA MBINGA AWAJIA JUU VIONGOZI WA KIJIJI CHA KIHUNGU

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbinga, Beda Hyera akizungumza kwa ukali mara baada ya kuchukizwa na viongozi wa kijiji cha Kihungu kata ya Kihungu katika Halmashauri ya mji wa Mbinga, kushindwa kusimamia ipasavyo ujenzi wa Ofisi ya kijiji hicho ili iweze kukamilika ujenzi wake kwa wakati.


Na Mwandishi wetu,
Mbinga.

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma, Beda Hyera amewajia juu baadhi ya viongozi wa kijiji cha Kihungu katika kata ya Kihungu Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani humo kutokana na kushindwa kukamilisha ujenzi wa Ofisi ya kijiji hicho.

Kufuatia hali hiyo, Hyera ametoa siku saba kwa viongozi hao kuhakikisha kwamba wanasimamia na kukamilisha ujenzi huo mapema iwezekanavyo, kuanzia Februari 5 mwaka huu kwani wananchi walikwisha changia fedha na uongozi wa Halmashauri hiyo ulitoa vifaa vya kiwandani kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo.

Hyera aliwanyoshea kidole viongozi wa kijiji hicho ambao ni Mwenyekiti wa kijiji Adam Ngongi na Mtendaji wa kijiji Denice Ndunguru kuwa ndiyo wanaokwamisha ujenzi huo usiweze kuendelea ipasavyo kutokana na kutunishiana misuli kwa sababu zisizokuwa na maana.


Hayo yalisemwa na Mwenyekiti huyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika juzi katika kata ya Kihungu, kwenye kilele cha maadhimisho ya sherehe ya kuzaliwa kwa CCM na kutimiza miaka 41 zilizofanyika kiwilaya katika kata hiyo.

Katika kuadhimisha sherehe hizo viongozi wa Chama cha mapinduzi wakiongozwa na Mwenyekiti huyo wa chama hicho waliweza kukagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi hiyo ambayo yamefikia katika hatua ya ujenzi wa ringbim ili iweze kuezekwa, ujenzi wa Ofisi ya CCM ya kata ambayo imefikia hatua ya kuezeka bati pamoja na ujenzi wa kituo cha afya Kalembo kilichopo katika kata hiyo.

“Watendaji wa Serikali waliokwamisha ujenzi wa Ofisi hii ya kijiji nimemwagiza Mkurugenzi mtendaji achukue hatua, ili mradi ule pale ulipofikia ndani ya siku saba uwe umekamilika ujenzi wake”, alisema Hyera.

No comments: