Tuesday, February 6, 2018

WANAFUNZI MKINGA SEKONDARI WATAKIWA KUONGEZA JUHUDI KATIKA MASOMO

Viongozi wa Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilayani Mbinga wakishirikiana na Walimu na Wanafunzi wa shule ya Sekondari Mkinga iliyopo Wilayani humo, kupanda miti katika eneo la shule kwa lengo la kutunza mazingira ya shule hiyo.


Viongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbinga, wakiwa katika picha ya pamoja Wanafunzi na Walimu wa shule hiyo.


Na Kassian Nyandindi,        
Mbinga.

WANAFUNZI wanaosoma katika shule ya Sekondari Mkinga Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kuongeza juhudi kwenye masomo yao ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao na kutimiza malengo waliyonayo katika maisha yao.

Aidha imeelezwa kuwa wametakiwa kuacha kujiingiza kwenye matendo maovu ambayo yanaweza kuwaharibia ndoto ya maendeleo ya masomo yao na maisha kwa ujumla.

Ushauri huo ulitolewa kwa nyakati tofauti na Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilayani humo, Sostenes Nchimbi na Katibu wa umoja huo Wilayani hapa, Daima Nyoni wakati walipokuwa wakizungumza juzi na wanafunzi wa shule hiyo.


Mazungumzo hayo yalienda sambamba mara baada ya watoto hao kushirikiana na viongozi hao wa CCM ambao walikuwa wameambatana na Wajumbe wengine wa Wilaya wa jumuiya hiyo kwenda kupanda miti katika eneo la shule hiyo kwa lengo la kutunza mazingira.

Zoezi hilo lilienda sambamba na maadhimisho ya kuzaliwa kwa Chama hicho na kutimiza miaka 41 sherehe ambazo ziliambatana na shughuli za kijamii ikiwemo upandaji miti uliofanywa na Jumuiya hiyo. 

Nchimbi alisema kuwa Wilaya ya Mbinga ni moja kati ya Wilaya chache hapa nchini zenye fursa nyingi ambazo zinatoa nafasi kwa vijana kujiendeleza zaidi kielimu, kwani hata historia inaonesha kuna idadi kubwa ya viongozi waliosoma na kushika nafasi za juu hapa nchini lakini tatizo baadhi ya vijana wenyewe hawataki kujituma na kuzingatia masomo yao.

“Nawasihi sana vijana ongezeni juhudi katika masomo yenu tumieni muda huu mlionao kujiandaa na masomo ya juu zaidi badala ya kuridhika na hapa mlipofikia kwani kumbukeni elimu haina mwisho”, alisema Nchimbi.

Naye Katibu wa Jumuiya hiyo ya Wazazi Wilaya ya Mbinga, Daima Nyoni aliongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo imeanza kufungua milango ya uwekezaji, hivyo inahitaji wasomi wengi watakaofanya kazi katika sekta mbalimbali na wale ambao wenye elimu ya juu.

Pamoja na mambo mengine, aliwataka wajitambue na kuelewa kuwa vijana ndiyo nguzo kuu ya uchumi katika nchi hivyo ni vyema wanapaswa kusoma kwa bidii ili taifa katika vizazi vijavyo liweze kupata wasomi wengi zaidi na wazalendo, jambo ambalo litasaidia kuwa na wataalam wengi na kuokoa kiasi kikubwa cha fedha wanacholipwa wataalam hao ambao ni wa fani mbalimbali kutoka nje ya nchi.

No comments: