Tuesday, February 27, 2018

TARURA TUNDURU YAPONGEZWA KUPUNGUZA KERO VIJIJINI



Na Muhidin Amri,     
Tunduru.

WANANCHI wa kijiji cha Kalulu kata ya Kalulu Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma, wameipongeza Serikali kwa jitihada zake inayofanya katika kupunguza kero za muda mrefu zinazokwamisha kasi ya ukuaji wa maendeleo kwa wananchi vijijini Wilayani humo.

Aidha wananchi hao wamepongeza kazi kubwa zinazofanywa na Meneja wa Wakala wa Barabara (TARURA) Mhandisi, Cyprian Kimwaga kwa kutengeneza barabara inayoanzia kijiji cha Milonde hadi Kalulu Wilayani hapa, kwa kiwango cha changarawe jambo ambalo limewezesha magari kuanza kupita kwenda katika vijiji hivyo ambapo ni muda mrefu yalikuwa yanashindwa kwenda huko kutokana na barabara hiyo kuwa na hali mbaya.

Wakizungumza na kwa nyakati tofauti, jana baadhi ya wananchi walisema kuwa usimamizi na mipango ya TARURA Wilayani Tunduru imefanikisha kutengenezwa kwa barabara hiyo ambayo kwa muda mrefu ilikuwa kero kubwa katika jamii.


“Kwa kweli lazima tukubali tangu Serikali yetu ilipoanzisha Wakala wa Barabara TARURA kumekuwa na mabadiliko makubwa ya kuimarika kwa miundombinu ya barabara katika kijiji chetu, tunafurahi kuona magari yanafika kwa wingi katika kijiji hiki kwa ajili ya kutoa huduma za usafiri, tunaipongeza sana Serikali yetu”, alisema Said Kalolo mkazi wa kijiji cha Kalulu.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala huyo wa barabara Wilayani Tunduru, Cyprian Kimwaga aliongeza kuwa ukarabati wa barabara hiyo umefanyika kwa juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dokta John Pombe Magufuli, kwa uamuzi wake wa kutoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa barabara hiyo na nyingine katika Wilaya hiyo.

Kimwaga alisema kijiji cha Kalulu kina umuhimu mkubwa kwani ni moja kati ya maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao mbalimbali ya chakula na biashara ambayo ndiyo yanaingiza mapato makubwa kwa Halmashauri ya Wilaya hiyo na Serikali kwa ujumla.

No comments: