Thursday, February 15, 2018

ASKOFU DALLU AVITAKA VYOMBO VYA DOLA KUZINGATIA UTOAJI HAKI



Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

ASKOFU wa Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Songea, Damian Dallu amesema kwamba suala la kuombea amani hapa nchini halitaweza kufanikiwa, endapo kama vyombo vya dola havitazingatia utoaji wa haki kwa wananchi wake.

Dallu alisema hayo jana wakati alipokuwa akihubiri kwenye ibada ya misa takatifu ya Jumatano ya majivu, iliyofanyika katika Kanisa kuu la kiaskofu la mtakatifu Mathias Kalemba mjini Songea.

Alisema kuwa amani haiwezi kupatikana katika taifa lolote lile kama vyombo vya dola havitatenda haki kwa wananchi wake, huku akidai kuwa ili amani iweze kudumishwa na kuwa endelevu ni lazima vyote viwili viende kwa pamoja.


Vilevile Askofu huyo amewataka waumini hao kuanzia ngazi ya familia, ofisi, taasisi mbalimbali pamoja na vyombo hivyo vya dola kuhakikisha vinatoa haki sawa kwa wananchi, watumishi na wafanyakazi wao mbalimbali kwa lengo la kudumisha amani iliyopo na mshikamano huu tulio nao.

Alisisitiza kuwa suala la kudumisha amani linatakiwa lianzie ndani ya mioyo ya watu na sio kuzungumzia mdomoni peke yake, badala yake ijidhihirishe kwa vitendo ikiwa pamoja na kutenda haki kwa wananchi wake.

Kadhalika kufuatia hali hiyo aliwaomba waumini hao kutumia kipindi hiki cha mfungo wa Pasaka kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye mahitaji muhimu wakiwemo watoto yatima, wafungwa, wagonjwa pamoja na wazee wasiojiweza.

Pia Askofu Dallu aliendelea kuwaasa waumini hao kutumia kipindi cha kwaresma kwa ajili ya kuachana na mambo ya anasa na kujinyima mahitaji yao muhimu ambapo amedai kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuwasaidia watu hao wenye mahitaji muhimu ambao hawajiwezi.

No comments: