Sunday, February 4, 2018

TLS YAWANYOSHEA KIDOLE WATUMISHI WA MAHAKAMA



Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa pamoja na Mahakama kupewa ridhaa ya kusimamia na kutoa haki kwa Wananchi, lakini kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya watumishi wa Mahakama wamekuwa wakikiuka sheria na taratibu za utumishi wa umma.

Aidha kufuatia hali hiyo wanatakiwa sasa kubadilika kwa kutenda haki, kufanya kazi kwa weledi, umakini na uadilifu wa hali ya juu kwa mujibu wa sheria za nchi.

Hayo yalisemwa na Mwakilishi wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) Wilaya ya Mbinga, Job Mwalukosya kwenye maadhimisho ya siku ya sheria nchini ambayo yalifanyika hivi karibu Februari 1 mwaka huu, katika majengo ya Mahakama ya Wilaya hiyo yaliyopo mjini hapa. 


Mwalukosya alifafanua katika hotuba yake kwamba kauli mbiu ya mwaka huu inaitaka idara ya Mahakama kuzingatia, “Matumizi ya Tehama katika utoaji wa haki kwa wakati na kwa kuzingatia maadili”.

Kufuatia hilo alisisitiza kuwa kauli mbiu hii inawataka Mahakama na Wadau wengine wa huduma za haki, kuhakikisha kuwa wanatekeleza majukumu yao ipasavyo katika kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi kwa haraka pasipo na vikwazo, kwa kuhakikisha kila wanachokifanya kuhusiana na utoaji haki kiwe kinazingatia manufaa ya wananchi.

Pamoja na mambo mengine, alieleza kuwa Mahakama kwa kushirikiana na Wadau hao inalojukumu la kutoa elimu kwa umma kuhusiana na matumizi hayo ya mfumo Tehama, katika utoaji haki ili kupambana na vitendo vinavyokiuka maadili ya utendaji kazi hususan rushwa na jeuri ya madaraka ya kimahakama kwa kuwa mfumo huo huweza kuleta ushahidi sahihi, hutunza siri na kutoa huduma husika kwa wakati.

Pia alibainisha kuwa Serikali kwa nafasi yake inapaswa kuzingatia kutoingilia uhuru wa Mahakama na vilevile inaowajibu wa kuziwezesha katika kuziongezea bajeti ya kutosheleza na kutoa elimu, ili ziweze kutumia mfumo wa Tehama vizuri katika utoaji haki kwa wakati na kukabiliana na changamoto ya msongamano wa mashauri Mahakamani.

Aliongeza kuwa kwa upande wa Mawakili na Polisi pia nao wanaowajibu wa kusimamia upatikanaji wa haki za wananchi bila kuvunja haki za binadamu huku wakiepukana na vitendo vya kuwabambikizia kesi wananchi, utoaji wa rushwa na uonevu katika mlolongo mzima wa kusimamia haki.

Vilevile askari Magereza nao wanaowajibu katika kusimamia haki za wafungwa kwamba zinalindwa, hivyo wanapaswa kuwasaidia pia kwa wale wanaotaka kukata rufaa wakiwa gerezani, kuwasiliana na Mawakili au ndugu zao kwa kuhakikisha nia zao za ukataji rufaa hazizuiliwi.

Wapo wasaidizi wa kisheria (Paralegals) na vyombo vya habari wanaowajibu nao wa kuzingatia wanasaidia wananchi, elimu ya matumizi ya Tehama katika utoaji haki kwa wakati inawafikia wananchi hao kupitia vyombo hivyo.

Na kwa upande wao wananchi wanapaswa kutambua kuwa Mahakama ni chombo huru na kipo kwa ajili yao katika kutoa haki, hivyo wanashauriwa kukitumia kwa ajili ya kupata haki.

No comments: