Tuesday, February 13, 2018

ROTALY CLUB NA MIKAKATI YA UTUNZAJI MAZINGIRA SONGEA

Baadhi ya viongozi wa Rotaly Club, tawi la Songea Mkoani Ruvuma wakiangalia kitalu kimojawapo cha miche ya miti kilichooteshwa na Club hiyo, ili miti iweze kusambazwa katika shule za msingi na sekondari katika Manispaa ya Songea Mkoani hapa.

Rais wa Rotaly Club tawi la Songea, Albert Kessy wa pili kushoto akiwa pamoja na baadhi ya viongozi wenzake wa Club hiyo wakikabidhi miche ya miti kwa Mratibu wa asasi isiyokuwa ya kiserikali aliyekuwa katikati ya Roots and shoots, Oddo Ngatunga inayofanya kazi ya uelimishaji kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari Mkoani Ruvuma juu ya masuala ya uhifadhi wa mazingira kwa jamii.


Na Muhidin Amri,     
Songea.

BAADHI ya shule za Msingi na Sekondari zilizopo katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma, zimekabidhiwa aina mbalimbali ya miche ya miti kutoka kwa Rotaly Club tawi la Songea iliyopo mjini hapa ili waweze kuipanda kwenye maeneo yao, ikiwa ni lengo pia la kurudisha uoto wa asili na utunzaji wa mazingira katika shule hizo.

Miche hiyo ambayo imekabidhiwa ni ile ambayo imeoteshwa katika vitalu kwa shule hizo ambayo ni miti 4,000 kati ya 15,000 wanayotarajia kuiotesha katika msimu wa mwaka huu.

Rais wa Club hiyo tawi la Songea, Albert Kessy alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu ambapo alidai kuwa miti ambayo wanaizalisha kwenye vitalu hivyo ni ile aina ya matunda, mbao, kivuli na mapambo.


Alifafanua kuwa mpango walionao ni kuendelea kugawa miche mingi zaidi kwa shule hizo ili waweze kuipanda hasa katika maeneo ambayo yanauharibifu mkubwa wa mazingira.

Kessy alibainisha kuwa katika kipindi cha mwezi Novemba mwaka jana walifanya matembezi ya hiari, ambayo yalilenga kukusanya fedha kwa ajili ya kununua mbegu za miti hiyo ambazo zimesaidia kuendelea na zoezi la kuzalisha miche na kuigawa katika shule hizo.

Pia alieleza kuwa mbali na hilo Rotaly Club licha ya kuwa na Wadau hao wa mazingira katika Manispaa hiyo, imefanikiwa pia kukarabati miundombinu ya shule mbalimbali za msingi na sekondari mjini humo ikiwemo ujenzi wa choo kipya kwa matumizi ya wanafunzi katika shule ya sekondari Bombambili.

“Tumefanikiwa kukarabati miundombinu ya shule ikiwemo ukarabati wa matundu ya vyoo 16 na kujenga choo kipya katika shule ya sekondari Bombambali, ambapo kabla ya hapo wanafunzi wa kike na wavulana walikuwa wakijisaidia katika choo kimoja na kwamba mradi huu wa miti tunakusudia kufika maeneo ya shule zote katika Manispaa hii”, alisema Kessy.

Changmoto kubwa wanayokabiliana nayo hivi sasa ni uhaba wa fedha kwani kiasi cha fedha walichoanzishia mradi huo hivi sasa ni fedha ambazo wamechangishana kutoka kwa wanachama wa Club.

Mbali na mradi wa miti, Kessy aliongeza kuwa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani na chuo cha VETA Songea walifanikiwa kukusanya waendesha bodaboda na kuwapa mafunzo ya udereva na uendeshaji wa matumizi sahihi ya barabara, ambapo vijana 150 waliweza kupata leseni na vyeti baada ya kupata mafunzo hayo.

Kwa upande wake naye Mratibu wa shirika lisilokuwa la Serikali, Roots and shoots ambalo linajihusisha na masuala ya uelimishaji katika utunzaji wa mazingira kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika Manispaa ya Songea, Mwalimu Oddo Ngatunga alisema kuwa msaada huo wa miti utawasaidia kuweza kurudisha uhifadhi wa mazingira kwa shule hizo kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

No comments: