Saturday, February 10, 2018

TAKUKURU RUVUMA YAOKOA MAMILIONI YA FEDHA MISHAHARA HEWA

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Ruvuma, Yustina Chagaka.


Na Kassian Nyandindi,      
Songea.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Ruvuma, imeokoa zaidi ya shilingi milioni 25 ambazo zilitaka kutumika kama mishahara hewa na idara mbalimbali za Serikali Mkoani humo.

Yustina Chagaka ambaye ni Mkuu wa taasisi hiyo Mkoani hapa alisema hayo juzi wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari mjini hapa.

Chagaka alikuwa akitoa taarifa ya Mkoa wa Ruvuma katika kipindi cha miezi tisa iliyopita, ambapo alisema kuwa kati ya fedha zilizookolewa zaidi ya shilingi milioni 22 ni za sekta ya afya na milioni 3 ni kutoka sekta ya elimu.


Alifafanua kuwa katika kipindi hicho TAKUKURU ilipokea taarifa 221 kutoka kwa wananchi.

Alizitaja idara ambazo zinaongoza kulalamikiwa kuwa ni Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ambapo kuna taarifa za malalamiko 57, ardhi 41, mahakama 25, polisi 13, vyama vya siasa 11 na elimu 12.

Kadhalika aliongeza kuwa katika kipindi hicho wameweza kukagua pia miradi nane ya maendeleo inayohusu ujenzi wa miundombinu ya afya, elimu na maji yenye thamani zaidi ya shilingi bilioni 8.5.

Alisema kuwa katika baadhi ya miradi hiyo ilikuwa na viashiria vya ubadhirifu na mapungufu mengi, hivyo uchunguzi wa matumizi ya fedha za miradi hiyo umeanzishwa ili kuweza kubaini ni kiasi gani cha fedha hakikutumika ipasavyo katika miradi husika.

No comments: