Friday, February 9, 2018

DOKTA KIGWANGALLA AWAPATIA MTIHANI WAMILIKI WA HOTELI



Na Mwandishi wetu,

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dokta Hamis Kigwangalla amewataka wamiliki na waendeshaji wa hoteli za daraja la kati kumwandikia mapendekezo yatakayomwezesha kutoa uamuzi sahihi, juu ya namna wanavyoweza kuchangia mapato ya nchi.
Dokta Hamis Kigwangalla.

Akizungumza jijini hapa leo Dokta Kigwangalla alisema kuwa uchunguzi umebaini kuwa hoteli zenye hadhi ya kati na nyumba za kulala wageni maarufu 'Guest House' zimekuwa zikipokea watalii wengi kutokana na ubora wake unaochangiwa na unafuu wa bei.

Waziri huyo alieleza kuwa tafsiri ya watalii haimaanishi Wazungu pekee bali ni wageni wowote wanaotumia nyumba za kulala wageni, kutoka nje ya eneo hilo wakiwemo wanaofika kwa ajili ya mikutano na shughuli za biashara.

“Mnaweza kuniambia hoteli zetu zina hadhi ya chini kwa sababu bei ya chumba ni kati ya Shilingi 40,000 hadi 70,000 lakini tunafahamu hizi hoteli Wazungu wameshazijua na wanalala kwenye hoteli zenu na mnaweza kuanza kuwatoza kwa dola”, alisema Kigwangalla.


Alisema kuwa lengo la Serikali ni kuwawezesha kukusanya mapato yatakayosaidia kuipatia uwezo wa kuhudumia wananchi kwenye sekta mbalimbali ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya barabara, usambazaji wa huduma ya maji, elimu na afya.

Mmoja wa wamiliki wa hoteli hizo, Amani Charles kwa upande wake alisema wanakusudia mapendekezo watakayowasilisha kwa Dokta Kigwangalla baada ya kukubaliana yatawawezesha kufanyabiashara kwa njia nzuri badala ya kunyonywa kimapato kutokana na kutokuwepo usawa wa malipo.

Aliongeza kuwa mkanganyiko wa malipo unatokana na wao kutakiwa kulipa kwa dola ya Marekani 1.5 kwa kitanda, ambayo ni karibu ni sawa na Shilingi 2,000 wakati wateja wao wanalipa kwa fedha za Kitanzania huku uamuzi wa kulipa kwa kiwango maalumu kwa mwaka au kwa asilimia kulingana na wateja wanaolala.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alisema utaratibu ambao umewekwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Arusha utaendelea, kwa sababu Serikali imeweka malengo ya makusanyo na wale ambao ukadiriaji wa mapato yao umefanyika hivi karibuni utapatiwa majibu na Waziri wa Maliasili na Utalii.

No comments: