Thursday, March 1, 2018

KUTOZINGATIA USAFI CHANZO CHA KUENEA KIPINDUPINDU DC KUWASHUGHULIKIA WATENDAJI



Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

MKUU wa Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye amesema kwamba kuendelea kutokea kwa tatizo la mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu mpaka sasa katika kata ya Ukata, Litembo na Matiri kunasababishwa na wananchi wanaoishi kwenye maeneo hayo kutozingatia masuala ya usafi.
Cosmas Nshenye.

Aidha alieleza kuwa hali hiyo ya uchafu inatokana pia na Watendaji wa vijiji na kata hawatimizi majukumu yao ya kazi ipasavyo, ikiwemo kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuzingatia kanuni za usafi majumbani mwao.  

Hayo yalisemwa juzi na Mkuu huyo wa Wilaya wakati alipokuwa akizungumza na viongozi mbalimbali wa Wilaya hiyo, kwenye kikao cha tathimini ya elimu katika ukumbi wa Jimbo la Mbinga uliopo mjini hapa.


Nshenye alisema kuwa kufuatia uzembe huo unaofanywa huko umesababisha kutokea kwa vifo vya watu watatu, ambao wamefariki dunia kwa kipindupindu kwa nyakati tofauti tokea ugonjwa huo ulipoanza kujitokeza Januari 29 mwaka huu kwenye maeneo hayo.

Alisisitiza kuwa Watendaji hao wanapaswa kutumia nguvu katika kuwaelimisha wananchi hao ili taatizo hilo lisiweze kuendelea kuleta madhara na kwa yule anayekaidi achukuliwe hatua za kisheria.

“Serikali tumekuwa tukitumia gharama kubwa kupambana na ugonjwa huu lakini kama Watendaji wa vijiji na kata, mngesimamia ipasavyo watu wazingatie usafi katika maeneo yao wanayoishi hakika ugonjwa huu usingeweza kuendelea kusumbua, wakufanya kipindupindu kiishe ni sisi viongozi kutimiza majukumu yetu ya kazi ipasavyo”, alisema Nshenye.

Pia alisema kuwa badala yake Watendaji hao wamekuwa wakiwaachia Wahudumu wa afya peke yao wakihangaika namna ya kudhibiti ugonjwa huo, hivyo aliongeza kuwa kwa mtendaji ambaye anaona hataki kufanya kazi au kutekeleza majukumu aliyopewa na Serikali ni vyema aachie ngazi mapema kabla hajachukuliwa hatua za kinidhamu.

“Na mimi nisingependa tuishi kwa msuguano kila mmoja ajitathimini utendaji wake wa kazi, tuache kufanya kazi kwa mazoea”, alisisitiza.

Katika hatua nyingine alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Gombo Samandito kuhakikisha kuwa Waganga wote wa jadi wawe wamesajiliwa na kutambuliwa kisheria.

Nshenye alimpatia mwezi mmoja Mkurugenzi huyo ahakikishe amekamilisha kazi hiyo na kumpelekea Ofisini kwake idadi kamili ya Waganga hao waliopo Wilayani humo.

“Ukishapata idadi yao niletee Ofisini kwangu, ili niweze kuwatambua ni wangapi wana kibali na wale wasiokuwa na kibali”, alisema. 

No comments: