Sunday, March 11, 2018

WAKULIMA MBINGA WALIA NA UENDESHAJI KILIMO CHA ZAO LA KAHAWA

Kahawa ambayo ipo shambani kama hii, ikikosa pembejeo za kilimo kama vile madawa na mbolea huwa kama hivi baada ya kukosa virutubisho halisi na kushambuliwa na wadudu waharibifu.


Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

BAADHI ya Wakulima wanaozalisha zao la Kahawa Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma, wamesema kwamba hivi sasa wanashindwa kuendesha kilimo cha zao hilo kutokana na mfumo uliowekwa na Serikali wa vyama vya ushirika, kushindwa kuwakopesha pembejeo za kilimo wakulima hao kama vile madawa na mbolea.

Aidha kwa nyakati tofauti walisema kuwa ni vyema wakati Serikali inajipanga kutekeleza hilo, wangeruhusu kwanza Makampuni binafsi ambayo yalikuwa yakiwawezesha pembejeo hizo yangeendelea kusambaza kwa wakulima hao, huku wakisubiri mfumo wa ushirika ukiendelea kuimarishwa.

Walidai kuwa mfumo wa vyama vya ushirika sio kwamba wanaupinga, lakini imekuwa ni haraka mno kuyasitisha Makampuni hayo ambayo yalikuwa ni msaada mkubwa kwao, hivyo ni vyema ungetolewa muda kwanza na masharti kadhaa namna ya kuweza kusaidia wakulima hao.


“Hivi sasa imekuwa ni tatizo kwetu tunashindwa kununua pembejeo za kilimo kama vile mbolea na madawa ya kupuliza kwenye mashamba yetu, tulikuwa tunaiomba Serikali ingetupatia muda kwanza wakati inajipanga na utekelezaji wa jambo hili”, walisema wakulima hao.

Pia zaidi ya asilimia 60 ya wakulima wa kahawa Wilayani Mbinga, wengi wao wanaiomba Serikali ingeweza kulegeza kwanza masharti iliyoweka sasa, ili makampuni hayo yaweze kuwakopesha pembejeo hizo na kunusuru mazao yaliyopo kwenye mashamba yao yasiweze kuendelea kuathirika na magonjwa mbalimbali.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari wakiwemo wataalamu wa kilimo ndani ya Wilaya hiyo, nao wameeleza kuwa katika kipindi cha msimu wa mwaka huu vyama vya ushirika havitakuwa na uwezo wa kukopesha pembejeo hizo wakulima hao wa kahawa.

Walisema Serikali katika kipindi hiki inajipanga kwanza namna gani ya kuboresha vyama hivyo, ili hapo baadaye kuanzia mwakani ushirika uweze kuanza kujitegemea wenyewe namna ya kusaidia wakulima hao.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Cosmas Nshenye alipoulizwa juu ya hali hiyo alisema kuwa wanajipanga kutoa elimu kwa viongozi wa vyama vya ushirika ili waone ni namna gani viongozi hao wataweza kuhudumia wakulima.

Nshenye alipotakiwa kutolea ufafanuzi juu ya malalamiko ya wakulima hao kukosa pembejeo katika msimu huu alibainisha kuwa taratibu husika zitakapokuwa tayari, Halmashauri kwa kushirikiana na vyama hivyo vya ushirika vilivyopo Wilayani hapa wataweza kusaidia wakulima kwa kuwakopesha pembejeo za kilimo za zao hilo la kahawa.

“Tunajua ni kweli baadhi ya wakulima hawana uwezo wa kuhudumia mashamba yao, lakini ni lazima viongozi hawa wa vyama vya ushirika na wataalamu wa kilimo wajipange kwanza kuhudumia wakulima”, alisema Nshenye.

No comments: