Wednesday, March 14, 2018

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WAFUGAJI WALIOVAMIA HIFADHI MADABA


Na Kassian Nyandindi,      
Madaba.

WAFUGAJI waliovamia katika hifadhi ya Gesi Masowa, katika kijiji cha Kipingo kata ya Lituta Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma, wanatakiwa kuondoka mara moja kabla Serikali haijatumia nguvu na kuwachukulia hatua kali za kisheria.

Hayo yalisemwa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema wakati alipokuwa akizungumza na Wawakilishi wa wafugaji hao, Wenyeviti wa vijiji, Maafisa mifugo pamoja na viongozi wa Wilaya ya Madaba.

Mgema alisema kuwa Serikali inayo taarifa kuwa baadhi ya wafugaji wameingia katika jimbo la Madaba na kwenda moja kwa moja katika hifadhi zilizotengwa kwa ajili ya makazi ya wanyama na kufanya shughuli zao za ufuagaji, ambapo amewataka baada ya wiki moja kuanzia sasa wawe wameondoka na kwenda katika ranchi ya Ngadinda iliyopo Wilayani humo ambayo imetengwa na Wizara ya mifugo kwa ajili ya shughuli hizo za ufugaji.


Vilevile katika kipindi hicho alisisitiza kuwa mifugo yote iwe imepigwa chapa ili kuzuia uingizaji holela wa ng’ombe, kutoka maeneo mengine kwa kuwa kila Wilaya hapa nchini imekwisha tenga maeneo ya wafugaji.

Kadhalika amewaonya Wenyeviti wa vijiji kuhusiana na tabia ya kuwatoza fedha wafugaji, kwa kisingizio cha kuweka mpango wa matumizi bora ya ardhi hasa kwa wafugaji wanaotoka nje ya Wilaya hiyo.

Mkuu huyo wa wilaya amemuagiza Afisa mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba pamoja na Watendaji wa vijiji vya Lituta na Kipingo kwenda kwa wafugaji hao, ili kuangalia uwezekano wa kupata njia ambayo itatumika kupitishia mifugo yao na kwenda katika ranchi ya Ngadinda kwa ajili ya upigaji chapa ng’ombe  wao bila kuharibu mazao ya wakulima wengine mashambani.

Katika hatua nyingine, amemtaka Mwenyekiti wa kijiji cha Kipingo kuacha mara moja tabia ya kukumbatia wafugaji na kuwaingiza ndani ya hifadhi kwa lengo la kujinufaisha maslahi yake binafsi.

“Tunazo taarifa kuwa wewe Mwenyekiti unahusika na uingizaji wa mifugo katika hifadhi ile kwa maslahi yako binafsi, unawaambia wafugaji wasiondoke na wewe utawalinda nakushauri acha tabia hii mara moja tutakushughulikia”, alisema Mgema.

No comments: