Friday, March 30, 2018

UJENZI MACHINJIO YA KISASA SONGEA KUKAMILIKA NDANI YA MKATABA


Na Albano Midelo,     
Songea.

KATIKA Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma, Mradi wa machinjio ya kisasa unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa gharama ya shilingi zaidi ya bilioni tatu, unatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Juni 30 mwaka huu.

Mradi huo unajengwa katika kata ya Tanga iliyopo kwenye Manispaa hiyo hadi sasa umefikia karibu ya asilimia 80 ujenzi wake, ambapo Mkandarasi wa ujenzi wa mradi huo ni Kampuni ya Giraffe ambayo imeahidi kukamilisha kazi hiyo kabla ya tarehe ya mwisho wa mkataba ambao umeanzia Julai 2017 na kukamilika Julai 2018 mwaka huu.

“Imebakia mistari michache kukamilisha kuzungusha jengo lote kisha tunaanza kazi ya kuezeka machinjio, hadi mwishoni mwa mwezi Mei tunatarajia kazi itakuwa katika hatua za mwisho”, alisema.


Kamati ya Fedha na Uongozi ya Baraza la Madiwani la Manispaa ya Songea, tayari imekagua mradi huo na kujiridhisha na kasi ya ujenzi huku wakisema kuwa wanaamini atamaliza kazi hiyo kwa wakati uliopangwa kwa mujibu wa mkataba husika.

Manispaa hiyo imelalamikia pia hivi karibuni Televisheni moja binafsi imetangaza habari ambazo sio sahihi kwamba, ujenzi wa machinjio hiyo unasuasua na kwamba Mkandarasi yupo nyuma ya mkataba jambo ambalo wamesema kuwa sio la kweli na ni upotoshaji katika jamii.

Rai imetolewa kuwa wanahabari kuhakikisha kwamba kabla ya kutangaza au kuchapisha habari wanapaswa kufanya utafiti ikiwemo kwenda hadi eneo husika ili kuweza kupata ukweli wa habari husika na hatimaye kutoa taarifa sahihi.

No comments: