Saturday, March 10, 2018

AFARIKI DUNIA BAADA YA KUGONGANA USO KWA USO PIKIPIKI WALIZOKUWA WAKIENDESHA


Na Kassian Nyandindi,    
Tunduru

MTU mmoja aliyejulikana kwa jina la Masudi Namurumi (28) amefariki dunia, katika tukio la ajali ambayo ilihusisha Pikipiki mbili kugongana uso kwa uso.
 
Mashuhuda wa tukio hilo walieleza kuwa lilitokea katika eneo la makutano ya barabara iendayo kijiji cha Nandembo na Kitalo Wilayani Tunduru Mkoa wa Ruvuma.

Pamoja na ajali hiyo kusababisha kifo hicho, watu watatu wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya hiyo ambao walikuwa abiria katika Pikipiki hizo.

Imeelezwa kuwa hali zao ni mbaya, baada ya kupata majeraha sehemu mbalimbali za miili yao.


Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo walieleza kuwa tukio hilo lilitokea majira ya usiku na kwamba chanzo cha ajali hiyo kimetokana na na mwendo kasi wa madereva wa Pikipiki hizo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Gemini Mushy amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akieleza kuwa Polisi bado wanaendelea na uchunguzi.

Alisema kuwa wananchi ambao walishuhudia wakati hali hiyo inatokea walitorosha Pikipiki hizo na kwenda kuzificha, katika maeneo yasiyojulikana ingawa hivi sasa tayari wamekwisha pata kwanza namba ya Pikipiki ambayo ilikuwa ikiendeshwa na Marehemu, Masudi.

Kamanda Mushy amewataka wananachi ambao wanataarifa za eneo zilipofichwa Pikipiki hizo, watoe taarifa Polisi ili ziweze kuchukuliwa kwa ajili ya taratibu za kisheria.

Aliwataja majeruhi hao kuwa ni Rashid Seif ambaye alikuwa dereva wa Pikipiki ya pili, Asiatu Peter na Ally Msokolo ambao walikuwa abiria katika Pikipiki hiyo.

Mganga wa zamu Dokta Baraka Mmari, ambaye ameufanyia uchunguzi mwili wa Marehemu huyo alisema kuwa chanzo cha kifo chake, kimesababishwa na kupasuka kichwa baada ya ajali hiyo kutokea.

Akizungumzia hali za majeruhi hao, Dokta Mmari alisema kuwa hali zao zinaendelea vizuri na kwamba maafisa tabibu, wanaendelea na juhudi za kuwapatia matibabu ili kuweza kuokoa maisha yao.

No comments: