Thursday, March 29, 2018

TBA YAKABIDHI BWENI SEKONDARI YA WASICHANA SONGEA

Na Kassian Nyandindi,     
Songea.
 
WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) wamekabidhi jengo moja, ambalo ni bweni la kulala wanafunzi katika shule ya Sekondari ya Wasichana Songea iliyopo Mkoani Ruvuma, ambalo limekarabatiwa kwa zaidi ya shilingi Milioni 102.

Kabla ya kukabidhi jengo hilo umefanyika ukaguzi wa bweni hilo ambalo ni la ghorofa likiwa na uwezo wa kuchukua Wanafunzi 110.

Ukaguzi huo uliwashirikisha watalaamu kutoka Manispaa ya Songea wakiwemo na mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Frowin Komba, Mhandisi wa ujenzi Karoline Kandonga, Mkuu wa shule hiyo Tupoke Ngwala, Mwakilishi wa TBA Mhandisi Eugenics Thomas na viongozi wa Serikali ya wanafunzi katika shule ya Sekondari ya Wasichana Songea.


Akizungumza juzi baada ya kukabidhi mradi huo mwakilishi wa TBA Mhandisi Eugenics Thomas alisema kuwa ukarabati wa bweni hilo ulianza Januari 10 mwaka huu na kwamba, ukarabati wa mabweni mengine matano unaendelea kufanywa shuleni hapo kwa awamu ambapo ukarabati wa bweni la pili utaanza rasmi mwezi Aprili mwaka huu.

Vilevile alitoa rai kwa wanafunzi wa shule hiyo ya Sekondari ambao wataingia katika bweni hilo lenye vitanda 110 na makabati 110 kuhakikisha kwamba wanatunza bweni hilo liwe wakati wote katika hali nzuri ya usafi kwa kuwa Serikali imetumia fedha nyingi za kukarabati.

Kwa upande wake Mkuu wa shule ya Sekondari ya Wasichana Songea, Tupoke Ngwala alisema Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya kufanyia ukarabati majengo yote ya shule hiyo, yakiwemo mabweni na majengo ya utawala.

Shule ya Sekondari ya Wasichana Songea ni miongoni mwa shule kongwe hapa nchini, ina wanafunzi 874 wanaosoma kidato cha tano na sita ambayo ilianzishwa mwaka 1974.

No comments: