Monday, March 5, 2018

SERIKALI YATENGA FEDHA TRILIONI MOJA KULIPA MADENI

Dokta Hassan Abbasi.


Na Mwandishi wetu,

SERIKALI imetenga jumla ya shilingi trilioni 1 kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 kwa ajili ya kuweza kulipa madeni mbalimbali ya watoa huduma, wazabuni na watumishi wa umma.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Dokta Hassan Abbasi alisema hayo leo mjini Dodoma, wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari juu ya utekelezaji wa miradi na ahadi mbalimbali za Serikali.

“Kati ya shilingi trilioni 1 zilizotengwa kulipia madeni kwa mwaka huu wa fedha, shilingi Bilioni 896.3 zimeshalipwa kwa watoa huduma, wazabuni na watumishi wa Serikali”, alisema Dokta Abbasi.


Alisema hesabu hiyo inajumuisha shilingi Bilioni 43 ambazo zimelipwa mwezi Februari mwaka huu, ikiwa ni malimbikizo ya wafanyakazi wa sekta ya umma.

“Madeni mengine ni uhakiki ambao unaendelea na yataendelea kulipwa siku zijazo na tutawajulisha”, alifafanua Dokta Abbasi.

Vilevile aliongeza kuwa Serikali itawaondolea adha ya usafiri wananchi wa maziwa makuu likiwemo Ziwa Nyasa, Tanganyika na Victoria. 

Kwa upande wa Ziwa Victoria, mkandarasi amepatikana na majadiliano ya mwisho na kusaini mkataba na kampuni ya STX ya Jamhuri ya Korea vitafanyika mwezi huu kwa ajili utengenezaji wa meli mpya itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200 na mizigo tani 400.

Kwa upande wa Ziwa Tanganyika zabuni kwa ajili ya utengenezaji wa meli mpya ya abiria na mizigo itatangazwa mwezi huu. 

Meli hiyo mpya itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo na italeta mapinduzi makubwa katika usafiri ziwani humo.

Kadhalika Dokta Abbasi alieleza kuwa mwezi Julai mwaka huu hapa nchini watapokea ndege kadhaa mpya ikiwemo Boeing Dreamliner na ukarabati wa viwanja vya ndege vya Kitaifa, Kimataifa na Kimkoa unaendelea kwa kasi kote nchini.

No comments: