Tuesday, March 27, 2018

HOMA YA NGURUWE BADO TISHIO IMEUA 864 SONGEA

Ugonjwa wa Nguruwe, unavyoteketeza Nguruwe Songea Mkoani Ruvuma.
Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

KATIKA Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma, wamesitisha uchinjaji wa Nguruwe katika maeneo yote ya Manispaa hiyo, tangu mwezi Februari mwaka huu, kufuatia kuibuka kwa homa ya Nguruwe ambayo haina kinga wala tiba.

Takwimu ambazo zimetolewa na Afisa Mifugo na Uvuvi wa Manispaa ya Songea, Bilaly Mwegeni zinaonesha kuwa homa hiyo ambayo inafahamika kwa jina la “African Swine Fever” katika kipindi cha kuanzia Januari 31 hadi Machi 14 mwaka huu imeua Nguruwe 864.

Mwegeni alisema kuwa takwimu hizo za vifo ni matukio ambayo yameripotiwa katika idara yake, ambapo uchunguzi umebaini kuwa zaidi ya nusu ya Nguruwe waliopo katika Manispaa hiyo wamekufa kutokana na ugonjwa huo, hali ambayo inahatarisha kuteketeza Nguruwe katika Manispaa hiyo.


“Takwimu zinaonesha kuwa Manispaa ya Songea ina Nguruwe 4,581 tukifanya sensa ya idadi ya Nguruwe waliobakia katika Manispaa yetu, naamini watakuwa hawazidi 2,000 kwa sababu kuna Nguruwe wengi wamekufa na takwimu za vifo hazijaletwa hapa Ofisini kwangu”, alisema Mwegeni.

Pia Mwegeni alizitaja kata ambazo zinaongoza kwa vifo vya Nguruwe hao kuwa ni Ndilima Litembo vifo (334), Lizaboni (138), Msamala (90), Matarawe (66) na Ruhuwiko (34) na maeneo mengine vifo vya Nguruwe huwa sio zaidi ya Nguruwe watano.

Kutokana na kuenea kwa homa hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ameagiza Watendaji wote wa Mitaa na Kata kuanzia sasa wahakikishe hakuna mtu kuchinja, kuingiza au kusafirisha Nguruwe kutoka katika maeneo mbalimbali.

Kadhalika uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu umebaini kuwa homa hiyo ya Nguruwe ipo katika Halmashauri tatu za Mkoa wa Ruvuma, ambazo ni Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Wilaya ya Songea na Wilaya ya Nyasa.

Vilevile kutokana na hali hiyo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo imeitisha mkutano wa wadau wa sekta ndogo ya Nguruwe, Machi 26 mwaka huu na kukutana nao kwenye ukumbi wa Maliasili mkoa kwa lengo la kujadili mkakati wa kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo na namna ya kudhibiti ueneaji wake.

Ugonjwa huu wa Nguruwe kwa ujumla hauna kinga na kwamba kitaalamu hauna madhara kwa binadamu ambapo kitaalamu Nguruwe aliyekufa kwa ugonjwa huo anatakiwa kuzikwa katika shimo lililopuliziwa dawa ya kuteketeza virusi lenye urefu wa zaidi ya meta moja.

No comments: