Tuesday, March 20, 2018

WALIOPORA VIWANJA UWT MBINGA KUKIONA CHA MOTO

Upande wa kulia ni Katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Mbinga, Martina Katyale akikabidhi taarifa fupi ya maendeleo ya umoja huo Wilayani humo kwa Katibu Mkuu wa UWT Taifa, Amina Makillagi alipokuwa juzi Katibu huyo katika ziara yake ya siku mbili Wilayani hapa. 
Aliyesimama upande wa kulia ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Amina Makillagi akizungumza na baadhi ya Wanawake wa Wilaya ya Mbinga, ambao walikusanyika katika uwanja wa Masumuni uliopo mjini hapa ambapo alisisitiza kuwa kwa wale watu waliopora viwanja vya UWT wahakikishe wanavirudisha haraka kabla hawajachukuliwa hatua kali za kisheria.

Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Amina Makillagi amesema kwamba, Viwanja vyote ambavyo vina migogoro na ni mali ya umoja huo Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma, wale wote ambao wamekuwa wakivitaka wakidai kuwa ni vya kwao wavirudishe mapema kabla hawajachukuliwa hatua kali za kisheria.

Alisisitiza kuwa yeyote aliyepora mali za Umoja huo, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais Dokta John Pombe Magufuli atapelekewa ripoti ili waweze kushughulikiwa. 

“Popote walipo hao ambao wamepora viwanja vyetu warudishe mara moja hatutaki utani, niwasihi na kuwaomba waachane na ubinafsi warudishe mali zetu”, alisisitiza Makillagi.

 
Agizo hilo alilitoa juzi alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari mjini hapa huku akisisitiza kuwa palipokuwa na mali ya UWT wanao ushahidi wa kutosha kwamba, ndiyo mali ya Umoja huo hivyo anatambua kuwa Mahakama ndiyo chombo cha kisheria ambacho mwisho wa siku kitasimamia haki yao.

Makillagi alisisitiza kuwa katika wiki mbili kuanzia sasa anataka awe amepewa taarifa mezani kwake kwamba, viwanja vyote vya Umoja wa wanawake hapa nchini, vimepimwa vikisubiri tayari kupewa hati miliki ili kuondoa migogoro isiyokuwa ya lazima.

Amewataka Wakurugenzi katika Halmashauri husika kwa kushirikiana na viongozi wa UWT, wahakikishe wanatoa ushirikiano wa kutosha katika upimaji wa viwanja hivyo ili hapo baadaye viweze kuleta manufaa kwa jamii.

“Kufika wiki mbili nataka niwe nimepata majibu juu ya hili agizo langu nililolitoa kwa viwanja vyote ambavyo ni mali yetu akina mama wa umoja huu wa wanawake, tutaleta mwanasheria wa kushughulikia matatizo haya na gharama zote za kushughulikia hili tutalipa chama Jumuiya ya UWT”, alisema.

Pia Katibu huyo alitumia msemo akisema kuwa “mali bila daftari hupotea bila habari”, hivyo kuna kila sababu ya kudhibiti mali na mapato ya chama kupitia miradi mbalimbali, huku viongozi ndani ya chama wakitengeneza ratiba ya kutembelea wanachama katika maeneo yao wanayoishi kwani wanaCCM wanahitaji kusogelewa karibu.

Pamoja na mambo mengine alisisitiza kuwa mali zote ndani ya Chama zimekuwa zikimilikiwa na Baraza la Wadhamini Taifa, hivyo kazi ya baraza hilo ni kusimamia mali hizo na kuhakikisha kwamba hakuna inayopotea.

No comments: