Sunday, March 11, 2018

RC RUVUMA AWATAKA VIJANA BODABODA KUJIUNGA MAFUNZO YA MGAMBO



Na Mwandishi wetu,    
Songea.

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mndeme amewataka Vijana ambao wanajihusisha na biashara ya kuendesha Pikipiki maarufu kwa jina la Bodaboda Mkoani humo kujiunga na mafunzo ya Mgambo ili waweze kukabiliana na vitendo vya uhalifu, hasa wanavyofanyiwa na watu wenye nia mbaya ambao wamekuwa wakitumia nafasi hiyo kuwanyang’anya Pikipiki zao ikiwa ndiyo njia rahisi ya kutekeleza uhalifu wao.
Christine Mndeme.

Mndeme alisema kuwa Serikali ya Mkoa itahakikisha kwamba inatoa mafunzo ya mgambo kwa vijana wote watakaokuwa tayari, ili kuweza kuwapata vijana wengi ambao watakuwa na mchango mkubwa katika masuala ya ulinzi na usalama ndani ya Mkoa na nchi kwa ujumla.

Alitoa kauli hiyo jana akiwa katika uwanja wa michezo wa Majimaji mjini Songea, wakati alipokutana na kuzungumza na vijana hao zaidi ya 200 waendesha Bodaboda kutoka maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Songea, huku akiwataka waachane na tabia ya ulevi na matendo maovu ambayo hayafai katika jamii.


Kadhalika aliwaeleza vijana hao waunge mkono, jitihada zinazofanywa na Rais Dokta John Pombe Magufuli katika kuhakikisha wanapiga vita vitendo vya wizi wa mali za umma, ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.

Katika hatua nyingine Mndeme amewataka pia waunde umoja wao na kuusajili kisheria, utakaoweza kuwasaidia kuwa na nguvu moja hasa katika shida na raha huku akiahidi kuwachangia shilingi Milioni 1 katika umoja huo ili waweze kufungua akaunti ya akiba benki.

Alisema kuwa kazi ya kuendesha Bodaboda ni kazi halali inayowapatia kipato cha kila siku, kama ilivyokuwa kazi nyingine hivyo vizuri wakajitambua na kupendana na sio kubaguana.

No comments: