Sunday, March 11, 2018

DOKTA MAGUFULI AWATAKA WAMILIKI WA VIWANDA VYA NDANI KUAJIRI WAZAWA



Na Mwandishi wetu,

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli amemwagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kuhakikisha kwamba wamiliki wote wa viwanda vya ndani wanaajiri wazawa.

Dokta Magufuli ametoa agizo hilo leo Machi 11 mwaka huu wakati alipokuwa akizindua kiwanda cha kufua vyuma cha Kahama Oil Mill kilichopo mjini Kahama Mkoa wa Shinyanga.

Alisema kuwa wananchi wazawa ndio waliompigia kura, hivyo ni lazima wapewe kipaumbele cha ajira katika viwanda hivyo.


“Kama wewe ni Waziri nimekuteua mimi, unaacha kuwaajiri wazawa walionipigia kura unaenda kuchukua watu wa nje ya nchi hii haikubaliki”, alisisitiza Dokta Magufuli.

Vilevile alitoa wito kwa mawaziri wote na wakurugenzi wahakikishe kwamba, viwanda vinavyoanzishwa hapa nchini wanaoajiriwa kwanza ni Watanzania.

Wamiliki wa viwanda wanapaswa pia kuhakikisha wanatumia malighafi za ndani kwanza kutengeneza bidhaa badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi.

“Mwaka huu pamba nyingi imelimwa, kahama Oil Mill pia mnatengeneza mafuta, hakuna haja ya kuagiza pamba kutoka nje wakati tuna pamba ya kutosha hapa”, alisema.

Kuhusu kiwanda cha chuma Dokta Magufuli alisema malighafi inapatikana nchini, hivyo iwapo Mkurugenzi wa Kahama Oil Mill anahitaji yupo tayari kumpa bure badala ya kuagiza nje.

Pamoja na mambo mengine, amewataka Watanzania kuwa na mazoea ya kununua bidhaa za ndani huku akiwataka wamiliki wa viwanda kutengeneza zenye ubora ili kuhimili ushindani wa kibiashara.

No comments: