Friday, March 30, 2018

WAPIGWA FAINI KWA KUKATAA KUCHANGIA FEDHA ZA USAFI WA MAZINGIRA


Na Muhidin Amri,   
Songea.

BAADHI ya Wakazi kumi wanaoishi katika maeneo mbalimbali Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma, wamepigwa faini ya shilingi Milioni moja kwa ujumla wao baada ya kubainika wamekataa kulipa shilingi 2,000 ambayo inatozwa kila mwezi kwa kila kaya, kwa ajili ya kuchangia huduma za usafi wa mazingira katika Manispaa hiyo.

Mahakama ya Mwanzo Mfaranyaki iliyopo mjini hapa, ndiyo iliyowahukumu adhabu hiyo na kwamba Wakazi hao ni wale wa kutoka katika kata ya Majengo, Misufini, Bombambili na Matarawe.

Philipo Beno ambaye ni Mkuu wa masuala ya usafi wa mazingira katika Mnispaa ya Songea akizungumza juzi na Waandishi wa habari, alisema kuwa wameamua kuanza kuwapeleka Mahakamani Wananchi wote wanaonekana kukaidi kulipa mchango huo, ili iweze kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo na hatimaye waweze kuchangia kwa urahisi bila usumbufu wowote kwa kufuata taratibu na sheria ndogo zilizowekwa.


“Sheria imepitishwa kwamba kila mwezi wanatakiwa kuchangia shilingi 2,000 kwa kila kaya na kwa upande wa Wafanyabiashara, hawa wanachangia shilingi 4,000 ili tuweze kufanya usafi wa mazingira kwa ufasaha kwenye mitaa na kata zetu zilizopo katika Manispaa hii”, alisema Beno.

Alifafanua kuwa baada ya kukataa kuchangia mchango huo, waliona ni vyema wapelekwe katika Mahakama hiyo ambako katika hao kumi kila mmoja alipigwa faini ya shilingi 100,000 huku akiongeza kuwa, kuanzia sasa zoezi la kuwapeleka Mahakamani litakuwa endelevu kwa wale wote watakaokuwa wakikaidi kutekeleza suala hilo.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema naye amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Songea Mkoani hapa, kupitia Maafisa wake wa afya kuendelea kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu zoezi la usafi wa mazingira kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi, ambayo ndiyo ni siku maalum ya kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya umma.

Alitoa agizo hilo huku akieleza kuwa wananchi wengi wa Songea wamekuwa hawashiriki kikamilifu katika siku hiyo ya usafi hivyo kwa wale wanaokaidi wanapaswa kuchukuliwa hatua.

Mgema amewaagiza pia Watendaji wa mitaa 95 iliyopo mjini hapa kuorodhesha majina ya wale wote wanaokataa kushiriki kufanya usafi huo wa mazingira, ili waweze kupigwa faini ya shilingi 50,000 kila mmoja kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.

Alisisitiza kuwa usafi wa mazingira ni jambo la lazima na sio hiari ili kuweza kukabiliana na magonjwa yanayosababishwa na uchafu na kwamba, utafiti umebaini kuwa nchi zilizoendelea hapa duniani zimekuwa zikishangaa kusikia au kuona watu wanaugua na kupoteza maisha kutokana na magonjwa yatokanayo na uchafu.

No comments: