Sunday, March 4, 2018

NAMTUMBO WATUMIA BILIONI 3.6 KUWEZESHA KAYA MASKINI



Na Yeremias Ngerangera,    
Namtumbo.

HALMASHAURI ya Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma, imetumia kiasi cha shilingi Bilioni 3.6 kuwawezesha wanufaika wa kaya maskini tangu mpango huo, ulipoanzishwa Wilayani humo mwaka 2015.

Raphael Mponda ambaye ndiye Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Wilayani hapa, alisema hayo juzi wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini hapa.

Alisema kuwa wameweza kuwalipa wanufaika hao kwa awamu 16 Wilayani Namtumbo tangu mpango huo uanzishwe.


Mponda alieleza kuwa mafanikio ya mpango huo kwa wanufaika wa kaya maskini kuwa ni pamoja na kaya 2,073 kati ya kaya 5,559 ambazo zimejiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).

Kufuatia utekelezaji huo mahudhurio ya watoto shuleni yameongezeka na kwamba kaya zinazonufaika zimeweza kuboresha pia makazi yao na watoto 181 waliopo kwenye kaya hizo wamehitimu darasa la saba mwaka 2017 na kuweza kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu.

Baadhi ya wanufaika wa kaya maskini, Zena Faraji kutoka kijiji cha Suluti na Ridhiki Issa wa kijiji cha Nahoro walidai kuwa mpango wa kunusuru kaya maskini, umeboresha maisha yao kutokana na kujikita zaidi katika shughuli za kilimo na kufuga mifugo iliyonunuliwa na fedha zinazotolewa na Serikali.

Wanufaika hao walidai kuwa wamejiunga katika vikundi vya kaya maskini vya kuweka na kukopa, ambavyo vinawawezesha kuweka fedha zao na kukopa fedha kwa ajili ya kufanya biashara ndogo ndogo.

Naye Kaimu Ofisa maendeleo ya jamii, Owigo Phinias pamoja na mambo mengine alisema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo ina vikundi 28 vya wanufaika wa kaya maskini ambapo baadhi ya vikundi vimefikia hatua ya kupata usajili baada ya kutimiza masharti husika, huku baadhi ya vikundi vingine vikiendelea na hatua ya usajili kwa lengo la kuwawezesha kukopa fedha katika mfuko wa wanawake unaotolewa na Halmashauri hiyo.

No comments: