Saturday, March 10, 2018

TATIZO LA UKATILI WA KIJINSIA CHANGAMOTO KUBWA WILAYA YA MBINGA

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mndeme ambaye amefunga kitambaa rangi ya njano kichwani akifurahi kwa pamoja mbele ya kundi la Wanawake wa Wilaya ya Mbinga Mkoani humo, siku ya maadhimisho ya Wanawake duniani ambapo katika Mkoa huo yalifanyika katika kijiji cha Lipumba kata ya Kihangimahuka Wilayani Mbinga. 

Upande wa kushoto aliyevaa kitambaa rangi ya njano kichwani ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mndeme akikagua moja kati ya mabanda ya maonesho siku ya maadhimisho ya Wanawake duniani ambapo katika Mkoa huo yaliadhimishwa Kimkoa katika kijiji cha Lipumba kata ya Kihangimahuka Wilaya ya Mbinga, na kwamba banda hilo ambalo ni la Dawati linaloshughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia Wilayani humo amelitaka kuhakikisha kwamba linatekeleza majukumu yake ipasavyo, ili kuweza kudhibiti matatizo ya ukatili wa kijinsia katika jamii.


Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

KUHUSU tatizo la Ukatili wa kijinsia unaofanywa dhidi ya wanawake, imeelezwa kuwa ni miongoni mwa changamoto kubwa inayoongoza katika Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma ambapo wanawake wamekuwa wakipigwa, kubakwa, kutelekezwa na kunyang’anywa mali zao hasa pale waume zao wanapofariki dunia.

Tatizo hilo hivi sasa limeongezeka na kukua kwa kasi ambapo katika mwaka 2016 kulikuwa na malalamiko ya ukatili wa kijinsia 232 ikiwemo miongoni mwao kesi za kubakwa 30 na kupigwa 105.

Imefafanuliwa kuwa wanawake wamekuwa hawashirikishwi katika kupanga mipango ya miradi ya maendeleo, katika familia na kupewa fursa ya kufanya maamuzi hivyo kufanya changamoto hiyo kuendelea kuwa kubwa.


Kufuatia hali hiyo Mkuu wa Mkoa huo, Christine Mndeme amelitaka Dawati linaloshughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia katika Wilaya ya Mbinga Mkoani humo, kutekeleza majukumu yake ipasavyo ili kuweza kudhibiti hali hiyo isiweze kuendelea kushamiri miongoni mwa jamii.

Mndeme alisema hayo juzi wakati alipokuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani, yaliyofanyika kimkoa katika kijiji cha Lipumba kata ya Kihangimahuka Wilayani hapa.

Alisema kuwa wananchi hususan kundi la wanawake wanapaswa kwa ujumla wao, kusaidia kutoa taarifa sahihi hasa pale inapotokea unyanyasaji au ukatili wa aina yoyote ile katika jamii.

“Kuhusiana na masuala ya ukatili wa kijinsia katika Mkoa huu Mbinga inaongoza, lakini pia hata sisi wazazi tujitahidi kuwalea watoto wetu wawe na maadili mema, maana jukumu la malezi ya watoto linaanzia ngazi ya familia tunawajibu kuhakikisha watoto wetu wanapata mahitaji yao ya msingi bila kuwabagua kwa misingi ya jinsia, ikumbukwe kwamba kumuelimisha mtoto wa kike ni kueelimisha taifa”, alisema Mndeme.

Alisisitiza kuwa wanawake wanapaswa kusaidia katika kuhakikisha amani na utulivu, vinakuwepo wakati wote miongoni mwa jamii na kukemea kwa nguvu zote aina yoyote ile ya ubaguzi pale unapojitokeza kwani Taifa linataka kuwa na watu wenye maadili mema, uwazi na uaminifu.

Kwa upande wake, Suzan Hyera ambaye ni Afisa Mtendaji wa kijiji cha Lipumba Wilayani Mbinga akisoma risala fupi kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Ruvuma, mbele ya Mkuu wa Mkoa huo alifafanua kuwa wanawake wanakabiliwa na changamoto kadha wa kadha ikiwemo vikundi vya wanawake na vijana, kukosa mikopo au kupewa mikopo kidogo kutoka kwenye taasisi za kifedha.

Hyera alizitaja changamoto nyingine kuwa ni wanawake wamekuwa wakitumikishwa katika kazi za kukuza uchumi ambazo matokeo yake ni kuwafaidisha wanaume, pembejeo za kilimo za ruzuku kutotolewa kwa wakati na pale zinapotolewa hutolewa kwa kiwango kidogo na kuuzwa kwa bei juu na kwamba vituo vya kutolea huduma ya afya kukosa waganga wenye sifa na badala yake wakunga ndio wanakuwa waganga wa vituo.

Alieleza kuwa kumekuwa na upungufu wa vituo vya kutolea huduma za kiafya katika kata ikiwemo uhaba wa vifaa tiba hasa kwa akina mama wajawazito na watoto, kwani hilo limekuwa ni tatizo katika Mkoa wa Ruvuma hasa kwa maeneo ya vijijini wamekuwa wakikosa hata miundombinu imara na salama ya maji ya bomba.

Pia aliongeza kuwa ili waweze kuwa na afya bora katika kuinua uchumi wa familia pamoja na Taifa kwa ujumla na kuweza kufikia kauli mbiu ya siku ya maadhimisho ya wanawake duniani isemayo; “Kuelekea uchumi wa viwanda tuimarishe usawa wa jinsia na uwekezaji wa wananchi vijijini” ni lazima sasa viongozi ndani ya Halmashauri za Wilaya wajitahidi kutunisha mfuko wa wanawake na vijana ili walengwa waendelee kupata mikopo yenye riba nafuu.

No comments: